Add parallel Print Page Options

Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu

(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Yh 1:19-28)

Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, ambapo:

Pontio Pilato alikuwa gavana wa Uyahudi;

Herode alikuwa mtawala wa Galilaya;

Filipo ndugu yake Herode alikuwa mtawala wa Iturea na Trakoniti;

na Lisania, alikuwa mtawala wa Abilene.

Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Katika kipindi hiki, Yohana, mwana wa Zakaria, alikuwa akiishi jangwani na alipata ujumbe kutoka kwa Mungu. Alipita katika maeneo yote yaliyo karibu na Mto Yordani akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. Hii ni kama maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya, yanayosema,

“Kuna mtu anayeipaza sauti yake kutokea nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
    nyoosheni njia kwa ajili yake.
Kila bonde litajazwa,
    na kila mlima na kilima vitasawazishwa.
Barabara zilizopinda zitanyooshwa,
    na barabara zenye mashimo zitasawazishwa.
Na kila mtu ataona
    jinsi Mungu atakavyowaokoa watu wake.’”(A)

Makundi ya watu walimwendea Yohana ili awabatize. Lakini aliwaambia, “Enyi nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? Badilisheni mioyo yenu! Kisha onesheni ya kuwa mmebadilika kwa namna mnavyoishi. Ninajua mtasema kuwa, ‘Ibrahimu ni baba yetu.’ Hilo halijalishi chochote. Ninawaambia Mungu anaweza kumwumbia Ibrahimu watoto kutokana na mawe haya! Na sasa shoka liko tayari kukata miti,[a] kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”

Read full chapter

Footnotes

  1. 3:9 miti Watu wasiomtii Mungu ni kama miti itakayokatwa.