Add parallel Print Page Options

Yohana Azungumza Juu ya Kristo

(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Lk 3:1-9,15-17)

19 Viongozi wa Kiyahudi kule Yerusalemu walituma baadhi ya makuhani na Walawi kwa Yohana kumwuliza, “Wewe ni nani?” Yohana akawaeleza kweli. 20 Akajibu kwa wazi bila kusitasita, “Mimi siyo Masihi.”

21 Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?”

Yohana akawajibu, “Hapana, mimi siye Eliya.”

Wakamwuliza tena, “Je, wewe ni Nabii?”[a]

Naye akawajibu, “Hapana, mimi siyo nabii.”

22 Kisha wakamwuliza, “Wewe ni nani basi? Tueleze habari zako. Tupe jibu la kuwaambia wale waliotutuma. Unajitambulisha mwenyewe kuwa nani?”

23 Yohana akawaambia maneno ya nabii Isaya:

“‘Mimi ni mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
    Nyoosheni njia kwa ajili ya Bwana.’”(A)

24 Wale Wayahudi walitoka kwa Mafarisayo. 25 Wakamwambia Yohana, “Unasema kuwa wewe siyo Masihi. Na unasema kuwa wewe siyo Eliya wala nabii. Sasa kwa nini unawabatiza watu?”

26 Yohana akajibu, “Nawabatiza watu kwa maji. Lakini yupo mtu hapa kati yenu ambaye ninyi hamumjui. 27 Yeye ndiye yule anayekuja baada yangu. Nami sina sifa za kuwa mtumwa anayefungua kamba za viatu vyake.”

28 Mambo haya yote yalitokea Bethania iliyokuwa upande mwingine wa Mto Yordani. Hapa ndipo Yohana alipowabatiza watu.

Read full chapter

Footnotes

  1. 1:21 Nabii Huenda walikuwa na maana nabii ambaye Mungu, alimwambia Musa ya kwamba atamtuma. Tazama Kum 18:15-19. Pia katika mstari wa 25.