Mzabibu Wa Kweli

15 ‘Mimi ni mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata; na kila tawi lizaalo, yeye hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya mafundisho nili yowapa. Kaeni ndani yangu nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda pasipo kuwa sehemu ya mzabibu, vivyo hivyo, ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kufanya lo lote. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; anayekaa ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa matunda mengi sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lo lote mtakalo nanyi mtatendewa. Mnapozaa matunda kwa wingi Baba yangu anatukuzwa, na hivyo mnadhihirisha kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.

“Kama Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivy owapenda ninyi; dumuni katika pendo langu. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa ndani ya pendo langu kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.

11 “Nimewaambia haya kusudi furaha yangu iwe ndani yenu, nanyi mpate kuwa na furaha iliyokamilika.

12 “Amri yangu ni hii: pendaneni kama nilivyowapenda. 13 Hakuna mtu mwenye upendo unaozidi ule wa mtu anayejitoa afe kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu ikiwa mtafa nya ninayowaagiza. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena kwa sababu mtumishi haelewi shughuli za bwana wake; bali nimewaita rafiki, kwa maana mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu nimewa fahamisha. 16 Hamkunichagua, bali mimi nimewachagua ninyi na nimewatuma mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu, ili lo lote mtakalomwomba Baba katika jina langu, awatimizie. 17 Hii ndio amri yangu: pendaneni.

18 “Kama ulimwengu ukiwachukia, fahamuni kwamba ulinichukia mimi kabla haujawachukia ninyi. 19 Kama mngekuwa watu wa ulim wengu huu, ulimwengu ungeliwapenda. Ulimwengu unawachukia kwa sababu ninyi si wa ulimwengu huu na mimi nimewachagua kutoka katika ulimwengu.

20 “Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi na ninyi pia watawatesa; kama wamelishika neno langu na neno lenu watalishika pia. 21 Lakini yote haya watawatendea kwa ajili yangu kwa sababu hawamfahamu Baba yangu ambaye amenituma. 22 Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia. Lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi zao. 23 Mtu ye yote anayenichukia mimi anamchukia na Baba yangu. 24 Kama nilikuwa sikuwafanyia miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine ye yote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini wameona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. 25 “Hali hii imetokea kama ilivyoandikwa katika Sheria kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’ 26 Lakini atakapokuja yule Msaidizi nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, yaani yule Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27 Na ninyi pia ni mashahidi wangu kwa maana tangu mwanzo mmekuwa pamoja nami.”

Yesu ni Kama Mzabibu

15 Yesu akasema, “Mimi ndiye mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Yeye hulikata kutoka kwangu kila tawi lisilozaa matunda.[a] Pia hupunguza majani katika kila tawi linalozaa matunda ili kuliandaa liweze kuzaa matunda zaidi. Ninyi mmewekwa tayari[b] kwa ajili ya kuzaa matunda[c] kutokana na mafundisho yale niliyowapa. Hivyo mkae mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nitakaa nikiwa nimeunganishwa kwenu. Hakuna tawi linaloweza kuzaa matunda likiwa liko peke yake. Ni lazima liwe limeunganishwa katika mzabibu. Ndivyo ilivyo hata kwenu. Hamwezi kutoa matunda mkiwa peke yenu. Ni lazima muwe mmeunganishwa kwangu.

Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Mtatoa matunda mengi sana mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nimeunganishwa kwenu. Lakini mkitenganishwa mbali nami hamtaweza kufanya jambo lo lote. Kama hamtaunganishwa nami, basi mtakuwa sawa na tawi lililotupwa pembeni nanyi mtakauka. Matawi yote yaliyokufa jinsi hiyo hukusanywa, hutupwa katika moto na kuchomwa. Hivyo ninyi mbaki mmeunganishwa nami, na mfuate mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, mnaweza kuomba kitu chochote mnachohitaji, nanyi mtapewa. Ninyi mdhihirishe kuwa mmekuwa wafuasi wangu kwa kutoa matunda mengi. Kwani hiyo itamletea Baba utukufu.[d]

Mimi nimewapenda kama vile Baba alivyonipenda. Sasa mdumu katika upendo wangu. 10 Nimezitii amri za Baba yangu, naye anaendelea kunipenda. Kwa jinsi hiyo, nami nitaendelea kuwapenda mkizitii amri zangu. 11 Nimewaambia haya ili mpate furaha ya kweli kama ile niliyonayo mimi. Nami ninatamani muwe na furaha iliyo kamilifu. 12 Hii ndiyo amri yangu kwenu: Mpendane ninyi kwa ninyi kama mimi nilivyowapenda. 13 Hakuna anayeweza kuonesha pendo lolote kuu zaidi ya kuwa tayari kufa kwa ajili ya rafiki zake. Upendo wa hali ya juu unaoweza kuoneshwa na watu ni kufa badala ya rafiki zao. 14 Nanyi ni rafiki zangu mnapoyafanya yale ninayowaambia myafanye. 15 Siwaiti tena watumwa, kwa sababu watumwa hawajui yale yanayofanywa na bwana zao. Lakini sasa nawaita marafiki, kwa sababu nimewaambia yote aliyoniambia Baba yangu.

16 Ninyi hamkunichagua mimi. Bali ni mimi niliyewachagua ninyi. Nami niliwapa kazi hii: Kwenda na kutoa matunda; matunda ambayo yatadumu. Ndipo Baba atakapowapa chochote mtakachomwomba katika jina langu. 17 Hii ndiyo amri yangu: Mpendane ninyi kwa ninyi.

Yesu Awatahadharisha wafuasi Wake

18 Endapo ulimwengu utawachukia, mkumbuke kwamba umenichukia mimi kwanza. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu huu, ulimwengu ungewapenda kama watu wake. Lakini ulimwengu unawachukia kwa sababu ninyi siyo wa ulimwengu huu. Badala yake, mimi niliwachagua ninyi ili muwe tofauti na ulimwengu.

20 Kumbukeni somo nililowafundisha: Watumwa sio wakubwa kuliko mabwana wao. Kama watu walinitendea mimi vibaya, watawatendea vibaya hata nanyi pia. Na kama waliyatii mafundisho yangu, watayatii hata ya kwenu pia. 21 Watawatendea yale waliyonitendea mimi, kwa sababu ninyi ni wangu. Wao hawamjui yeye aliyenituma. 22 Kama nisingekuwa nimekuja na kusema na watu wa ulimwengu, basi wasingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa nimekwisha sema nao. Hivyo hawana cha kisingizio cha dhambi zao.

23 Yeyote anayenichukia mimi anamchukia na Baba pia. 24 Mimi nilifanya mambo miongoni mwa watu wa ulimwengu ambayo hayajawahi kufanywa na mtu yeyote mwingine. Kama nisingefanya mambo hayo, wao nao wasingekuwa na hatia ya dhambi. Ijapokuwa waliyaona niliyofanya, bado wananichukia mimi na Baba yangu. 25 Lakini haya yalitokea ili kuweka wazi yaliyoandikwa katika sheria zao: ‘Walinichukia bila sababu yoyote.’”[e]

26 Mimi, “Nitamtuma Msaidizi kutoka kwa Baba. Huyo Msaidizi ni Roho wa kweli anayekuja kutoka kwa Baba. Yeye atakapokuja, atasema juu yangu. 27 Nanyi pia mtawajulisha watu juu yangu, kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.

Footnotes

  1. 15:2 lisilozaa matunda Kuzaa matunda inamaanisha jinsi wafuasi wa Yesu wanavyopaswa kuishi ili kuonesha kuwa wao ni wa Yesu. Tazama mstari wa 7-10.
  2. 15:3 mmewekwa tayari Ni kufanywa safi kwa njia ya kukatiwa matawi (Kiyunani “Kusafishwa”) ilivyoelezwa kwenye mstari wa 2.
  3. 15:3 kuzaa matunda Ni jinsi wafuasi wa Yesu wanavyopaswa kuwa ili kudhihirisha kuwa wao ni wa Yesu.
  4. 15:8 utukufu Au “heshima”. Tazama Utukufu katika Orodha ya Maneno.
  5. 15:25 Walinichukia bila sababu yoyote Maneno haya yanaweza kuwa yamenukuliwa kutoka katika Zab 35:19 au Zab 69:4.