Yesu Awaosha Miguu Wanafunzi Wake

13 Ilikuwa siku moja kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka duniani na kurudi kwa Baba yake umekaribia. Alikuwa amewapenda sana wafuasi wake hapa duniani, akawapenda hadi mwisho. Na wakati alipokuwa akila chakula cha jioni pamoja na wanafunzi wake, shetani alikuwa amekwisha kumpa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu. Yesu akijua ya kwamba Baba yake alikwisha mpa mamlaka juu ya vitu vyote; na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, alitoka mezani akaweka vazi lake kando, akajifunga taulo kiunoni. Kisha akamimina maji katika chombo akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa ile taulo aliyojifunga kiu noni. Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, wewe unaniosha miguu?” Yesu akamjibu, “Hivi sasa huelewi ninalofa nya lakini baadaye utaelewa.” Petro akamjibu, “La, hutaosha miguu yangu kamwe!” Yesu akamwambia, “Kama sitaosha miguu yako, huwezi kuwa mfuasi wangu.” Ndipo Petro akasema, “Kama ni hivyo Bwana, nioshe miguu yangu pamoja na mikono yangu na kichwa changu pia!” 10 Yesu akamwambia, “Mtu aliyekwishaoga ni safi mwili mzima naye hahitaji tena kunawa ila kuosha miguu tu. Ninyi nyote ni safi, isipokuwa mmoja.” 11 Yesu alifahamu ni nani angemsaliti, ndio sababu akasema, “Ninyi nyote ni safi, isipo kuwa mmoja.”

12 Alipomaliza kuwaosha miguu alivaa tena vazi lake, akarudi alipokuwa amekaa, ndipo akawaambia, “Je, mnaelewa maana ya jambo nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi, Mwalimu na Bwana, na hii ni sawa, kwani ni kweli. 14 Kwa hiyo ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewaosha miguu, ninyi pia hamna budi kuoshana miguu. 15 Mimi nimewaonyesha mfano, ili mtendeane kama nilivyowafanyia. 16 Ninawaambia hakika, mtumishi hawezi kuwa mkuu kuliko bwana wake; wala anayetumwa hawezi kuwa mkuu kuliko aliyemtuma. 17 Kwa kuwa sasa mnafahamu mambo haya, mtabarikiwa na Mungu ikiwa mtayafanya. 18 Siwazungumzii ninyi nyote. Ninawa fahamu wote niliowachagua. Maandiko yaliyotamka, ‘Yeye aliyekula chakula pamoja nami amekuwa msaliti wangu,’ hayana budi kutimia. 19 Ninawaambia mambo haya kabla hayajatokea ili yatakapotokea mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye Kristo. 20 Nawahakikishia kuwa mtu anayemkubali na kumpokea ye yote ninayemtuma, ananipokea mimi. Na mtu anayenikubali na kunipokea, anampokea Baba yangu ambaye amenituma.”

Yesu Anatabiri Kuwa Yuda Atamsaliti

21 Baada ya haya Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Ninawaambia wazi, mmoja wenu atanisaliti.” 22 Wanafunzi wake wakatazamana kwa wasiwasi, kwa kuwa hawakujua anamsema nani. 23 Mmoja wa wanafunzi ambaye Yesu alimpenda sana alikuwa amekaa karibu sana na Yesu. 24 Kwa hiyo Simoni Petro akamwashiria yule mwanafunzi akamwambia, “Tuambie, ni nani anayemsema.” 25 Yule mwanafunzi akimwegemea Yesu akamwambia, “Tafadhali Bwana tuambie, ni nani unayemzungumzia?” 26 Yesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya.” Kwa hiyo baada ya kuchovya ule mkate akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. 27 Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, shetani akamwingia moyoni. Yesu akamwambia Yuda, “Jambo unalok wenda kufanya, kalifanye haraka.’ ’ 28 Hakuna hata mmoja wa wale wengine waliokuwepo pale mezani aliyeelewa maana ya maneno aliy otamka Yesu. 29 Baadhi yao walidhani kwamba alikuwa anamwagiza akanunue vitu watakavyohitaji kwa ajili ya sikukuu au awape mas kini cho chote, kwa kuwa yeye alikuwa mtunza fedha. 30 Kwa hiyo mara baada ya kupokea ule mkate, Yuda alienda zake nje. Wakati huo giza lilikwisha ingia.

Yesu Anatabiri Kuwa Petro Atamkana

31 Yuda alipokwisha ondoka, Yesu akawaambia, “Wakati ume karibia ambapo watu wataona utukufu wangu mimi Mwana wa Adamu na kwa njia hii watu watauona utukufu wa Mungu. 32 Na ikiwa Mungu atatukuzwa, yeye atanipa mimi utukufu wake, na atafanya hivyo mara. 33 Wapendwa wangu, muda wangu wa kuwa pamoja nanyi umekar ibia kwisha. Mtanitafuta; na kama nilivyowaambia Wayahudi, nina waambia na ninyi: ‘ninapokwenda hamwezi kunifuata’. 34 Nina waachia amri mpya: pendaneni ninyi kwa ninyi. Kama mimi nilivy owapenda, na ninyi mpendane vivyo hivyo. 35 Kama mkipendana hivyo, watu wote watafahamu ya kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”

36 Simoni Petro akamwuliza, “Bwana, kwani unakwenda wapi?” Yesu akamjibu, “Ninapokwenda hamwezi kunifuata sasa, lakini mtanifuata baadaye.” 37 Petro akamwuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kufa kwa ajili yako.” 38 Yesu akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kutoa maisha yako kwa ajili yangu? Ninakwambia hakika ya kuwa, kabla jogoo hajawika, utakanusha mara tatu kwamba hunijui.”

Yesu Aiosha Miguu ya Wafuasi wake

13 Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Yesu alijua kwamba wakati wake wa kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ulikuwa umefika. Daima Yesu aliwapenda watu wa ulimwengu huu waliokuwa wake. Huu ulikuwa wakati alipowaonesha upendo wake mkuu.

Yesu na wafuasi wake walikuwa wakila chakula cha jioni. Ibilisi alikuwa tayari amekwisha kumshawishi Yuda Iskariote kumsaliti Yesu kwa maadui zake. (Yuda alikuwa Mwana wa Simoni.) Baba alikuwa amempa Yesu uwezo juu ya kila kitu. Naye Yesu alilifahamu hili. Alijua pia kuwa yeye alitoka kwa Mungu. Tena alijua kuwa alikuwa anarudi kwa Mungu. Kwa hiyo walipokuwa wakila,[a] Yesu alisimama na kulivua vazi lake. Akachukua taulo na kuifunga kiunoni mwake. Kisha akamimina maji katika bakuli na kuanza kuwaosha miguu[b] wafuasi wake. Kisha akaifuta miguu yao kwa taulo aliolifunga kiunoni mwake.

Akamfikia Simoni Petro, naye Simoni Petro akamwambia, “Bwana, huwezi kuiosha miguu yangu.”

Yesu akamjibu, “Huyaelewi ninayofanya hivi sasa. Lakini utayaelewa baadaye.”

Petro akasema, “Hapana! Huwezi kamwe kuniosha miguu yangu kamwe.”

Yesu akamjibu, “Kama sitakuosha miguu yako, basi hutakuwa miongoni mwa watu wangu.”

Simoni Petro akasema, “Bwana, utakapomaliza miguu, unioshe mikono na kichwa pia!”

10 Yesu akamwambia, “Baada ya mtu kuoga, mwili wake wote huwa safi. Anahitaji tu kunawa miguu. Nanyi mko safi, lakini sio nyote.” 11 Yesu alimjua yule atakayemsaliti mbele ya adui zake. Ndiyo maana alisema, “Sio wote mlio safi.”

12 Yesu alipomaliza kuwaosha miguu wafuasi, alivaa nguo zake na kurudi pale mezani. Akawauliza, “Je, mmelielewa nililowafanyia? 13 Mnaniita mimi ‘Mwalimu’. Tena mnaniita mimi ‘Bwana’. Hayo ni sahihi, kwa sababu hivyo ndivyo nilivyo. 14 Mimi ni Bwana na Mwalimu wenu. Lakini niliwaosha miguu yenu kama mtumishi. Hivyo nanyi mnapaswa kuoshana miguu yenu. 15 Nilifanya hivyo kama mfano. Hivyo nanyi mnapaswa kuhudumiana ninyi kwa ninyi kama nilivyowahudumia. 16 Mniamini mimi, watumishi huwa sio wakubwa kuzidi bwana zao. Wale waliotumwa kufanya jambo fulani sio wakubwa kumzidi yule aliyewatuma. 17 Sasa, mkielewa maana ya yale niliyotenda, Mungu atawabariki mkiyatendea kazi.

18 Nami sizungumzii habari zenu nyote. Nawafahamu watu wale niliowachagua. Lakini Maandiko yanapaswa kutimia kama yanavyosema: ‘Mtu aliyekula chakula pamoja nami amenigeuka.’[c] 19 Ninawaambia hili sasa kabla halijatokea. Hivyo litakapotokea, mtaweza kuamini kuwa MIMI NDIYE.[d] 20 Hakika nawaambieni, yeyote anayempokea mtu yule niliyemtuma ananipokea mimi pia. Na yeyote anayenipokea mimi humpokea pia yeye aliyenituma.”

Yesu Amtaja Atakayemgeuka

(Mt 26:20-25; Mk 14:17-21; Lk 22:21-23)

21 Baada ya Yesu kuyasema mambo haya, alisumbuka sana moyoni. Akasema kwa uwazi, “Mniamini ninaposema kwamba mmoja wenu atanisaliti kwa maadui zangu.”

22 Wafuasi wake wote wakatazamana wao kwa wao. Hawakuelewa kuwa Yesu alikuwa anamzungumzia nani. 23 Mmoja wa wafuasi wake alikaa karibu na Yesu na alikuwa amemwegemea. Huyu alikuwa yule aliyependwa sana na Yesu. 24 Simoni Petro akaonyesha ishara kwa mfuasi huyo amwulize Yesu alikuwa anamzungumzia nani.

25 Yule mfuasi alisogea karibu sana na Yesu na kumwuliza, “Bwana, ni nani huyo?”

26 Yesu akamjibu, “Nitachovya mkate huu kwenye bakuli. Mtu yule nitakayempa mkate huo ndiye mwenyewe.” Kwa hiyo Yesu akachukua kipande cha mkate, akakichovya, na akampa Yuda Iskariote, Mwana wa Simoni. 27 Yuda alipoupokea mkate ule, Shetani akamwingia. Yesu akamwambia Yuda, “Yale unayotaka kuyafanya, yafanye haraka!” 28 Hakuna hata mmoja pale mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia Yuda hayo. 29 Kwa vile Yuda ndiye aliyekuwa msimamizi wa fedha[e] zao,[f] baadhi yao walidhani kuwa Yesu alikuwa na maana kuwa Yuda aende kununua vitu ambavyo wangehitaji kwa ajili ya sherehe. Au walidhani kuwa Yesu alitaka Yuda aende na kuwapa maskini cho chote.

30 Yuda akaula mkate aliopewa na Yesu. Kisha akatoka nje mara hiyo hiyo. Wakati huo ulikuwa ni usiku.

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

31 Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa ni wakati wa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu. Na Mungu ataupokea utukufu kupitia kwake. 32 Kama Mungu hupokea utukufu kupitia kwake, atampa Mwana Utukufu kupitia kwake yeye mwenyewe. Na hilo litatimia haraka sana.”

33 Yesu akasema, “Watoto wangu, nitakuwa nanyi kwa kipindi kifupi tu kijacho. Nanyi mtanitafuta, lakini nawaambia sasa yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: Kule niendako ninyi hamwezi kuja.”

34 “Nawapa amri mpya: Pendaneni ninyi kwa ninyi. Mnapaswa kupendana kama mimi nilivyowapenda ninyi. 35 Endapo mtapendana ninyi kwa ninyi watu wote watatambua kuwa ninyi ni wafuasi wangu.”

Yesu Asema Petro Atamkana

(Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Lk 22:31-34)

36 Simoni Petro akamwuliza Yesu, “Bwana, unaenda wapi?”

Yesu akajibu, “Kule niendako hamwezi kunifuata sasa. Lakini mtanifuata baadaye.”

37 Petro akauliza, “Bwana, kwa nini nisikufuate sasa? Mimi niko radhi kufa kwa ajili yako!”

38 Yesu akajibu, “Je, ni kweli utayatoa maisha yako kwa ajili yangu? Hakika nakwambia, kabla jogoo hajawika, utasema mara tatu kwamba hunijui mimi.”

Footnotes

  1. 13:4 wakila Wafuasi walikuwa kwenye makochi, wakiwa wameegemea kushoto kwao, na wakitumia mikono ya kulia kufikia vyombo vilivyokuwa mezani, vilivyowekwa mbele ya makochi. Yesu akamimina maji kwenye “jagi” (Wayunani huelezea kuwa hiki kilikuwa chombo kilichotumika maalumu kwa kusudi hilo) na kisha akaenda akimpitia mmoja mmoja nyuma ya kochi, ambako miguu ya wafuasi ilikuwa imenyooshwa.
  2. 13:5 kuwaosha miguu Utaratibu wa kijamii wa karne ya kwanza, kwa sababu watu walivaa viatu vya wazi katika barabara za vumbi jingi. Ulikuwa ni wajibu wa unyenyekevu, kawaida uliofanywa na mtumishi. Pia katika mstari wa 6-14.
  3. 13:18 amenigeuka Amenigeuka kwa hali halisi ina maana ya kuwa “Ameinua kisigino chake dhidi yangu.” Imenukuliwa kutoka Zab 41:9.
  4. 13:19 MIMI NDIYE Hili ni kama Jina la Mungu lililotumiwa katika Agano la Kale. Tazama Isa 41:4; 43:10; Kut 3:14. Hata hivyo, Inaweza kuwa na maana ya “Mimi Ndiye”, maana yake “Mimi Ndiye Masihi”. Pia katika mstari wa 28,58.
  5. 13:29 msimamizi wa fedha Mtunzaji wa fedha. Wafuasi walikuwa kama kundi moja walipokea michango na kuitunza pamoja kwa ajili ya mahitaji yao na kwa kuwasaidia maskini ila mmoja wao alisimamia sanduku la fedha.
  6. 13:29 zao Kiongozi wa mambo ya fedha ni sawa na kusema kwamba yeye alikuwa anatunza mfuko wa fedha za wafuasi walizopata hata kwa kuchangiwa na watu wengine.