Kuwa Na Amani Na Mungu

Basi, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa kupitia kwake tumepata njia ya kufikia neema hii ambayo inatuwezesha kusimama imara, tukifurahia tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. Zaidi ya hayo, pia tunafurahia mateso yetu kwa sababu tunafahamu kuwa mateso huleta subira; na subira huleta uthabiti wa moyo; na uthabiti wa moyo hujenga tumaini. Tukiwa na tumaini hatuwezi kukata tamaa kwa sababu Mungu amekwisha kumimina upendo wake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ni zawadi tuliyopewa na Mungu.

Tulipokuwa tungali wanyonge, wakati aliochagua Mungu, Kristo aliwafia wenye dhambi. Ni vigumu sana kwa mtu kujitolea kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa yawezekana mtu akajitolea kufa kwa ajili ya mtu mwema. Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo ali kufa kwa ajili yetu.

Basi, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa damu yake, bila shaka atatuokoa kutoka katika ghadhabu ya Mungu. 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa maadui wa Mungu tulipatanishwa kwa kifo cha Mwanae, bila shaka sasa kwa kuwa tumepatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Si hivyo tu, bali pia tunamfurahia Mungu katika Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kwa ajili yake tumepokea upatanisho wetu.

Adamu Alileta Kifo, Yesu Ameleta Uzima

12 Kwa hiyo kama vile ambavyo dhambi iliingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na dhambi ikaleta kifo, na kwa njia hiyo kifo kikawajia watu wote kwa kuwa wote walitenda dhambi -

13 kwa maana kabla sheria haijatolewa dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi ambapo hakuna sheria. 14 Hata hivyo tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Musa, kifo kiliwatawala watuwote hata wale ambao dhambi zao hazikuwa kama uasi wa Adamu. Adamu alikuwa mfano wa yule ambaye angalikuja. 15 Lakini zawadi iliyotolewa bure haiwezi kulinganishwa na ule uasi. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya uasi wa mtu mmoja, basi neema ya Mungu na zawadi iliyotolewa kwa ajili ya mtu mmoja, Yesu Kristo, imemiminika kwa wingi zaidi kwa watu wengi. 16 Pia zawadi ya Mungu sio kama matukio ya ile dhambi ya mtu mmoja. Kwa maana hukumu iliyotokana na uasi huo ilileta laana, lakini zawadi iliyopatikana bure baada ya dhambi nyingi, inaleta haki ya Mungu. 17 Na ikiwa kutokana na uasi wa mtu mmoja kifo kilitawala kupitia huyo mtu mmoja, wale wanaopokea wingi wa neema na zawadi ya bure ya kuhesabiwa haki, watatawala zaidi sana katika maisha kwa ajili ya huyo mtu mmoja, Yesu Kristo. 18 Kwa hiyo, kama vile uasi wa mtu mmoja ulivyoleta hukumu kwa watu wote, hali kadhalika, tendo la haki la mtu mmoja linawafanya watu wote waachiliwe huru na kupewa uzima. 19 Na kama vile ambavyo watu wengi walifanywa kuwa wenye dhambi kwa ajili ya kutokutii kwa mtu mmoja, vivyo hivyo wengi watahesabiwa haki na Mungu kwa ajili ya utii wa mtu mmoja.

20 Sheria ililetwa ili dhambi iongezeke. Lakini dhambi ili poongezeka, neema iliongezeka zaidi. 21 Kama vile ambavyo dhambi ilitawala kwa njia ya kifo, vivyo hivyo neema ya Mungu iweze kutawala kwa njia ya haki, ikileta uzima wa milele katika Yesu

Kuhesabiwa Haki na Mungu

Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa njia ya imani.[a] Hivyo sote[b] tuna amani pamoja na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kupitia imani yetu, Kristo ametufungulia mlango kuingia katika neema ya Mungu, tunayoifurahia sasa. Na tunashangilia sana kwa sababu ya tumaini tulilonalo la kushiriki utukufu wa Mungu. Na tunafurahia matatizo tunayoyapitia. Kwa nini? Kwa sababu tunajua kuwa mateso hutufundisha kuwa jasiri kipindi kigumu. Na ujasiri huu ni uthibitisho kuwa tuko imara. Na uthibitisho huu unatupa tumaini. Na tukiwa na tumaini hili, hatutakata tamaa kamwe. Tunajua hili kwa sababu Mungu ameumimina upendo wake na kuijaza mioyo yetu kupitia Roho Mtakatifu aliyetupa.

Yote haya ni kweli kutokana na aliyoyafanya Kristo. Wakati sahihi ulipotimia, tukiwa hatuwezi kujisaidia wenyewe na tusioonyesha heshima yoyote kwa Mungu, yeye Kristo, alikufa kwa ajili yetu. Ni watu wachache walio tayari kufa ili kuokoa maisha ya mtu mwingine, hata kama mtu huyo ni mwema. Mtu anaweza kuwa radhi kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema sana. Lakini Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa bado ni wenye dhambi, na kwa hili Mungu akatuonyesha jinsi anavyotupenda sana.

Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Kristo. Hivyo kwa njia ya Kristo hakika tutaokolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu. 10 Nina maana kuwa tulipokuwa bado adui wa Mungu, Yeye alifanya urafiki nasi kwa njia ya kifo cha Mwanaye. Kutokana na ukweli kwamba sasa tumekuwa marafiki wa Mungu, basi tunaweza kupata uhakika zaidi kwamba Baba atatuokoa kupitia uhai wa Mwanaye. 11 Na si kuokolewa tu, bali pia, hata sasa tunafurahi kwa yale ambayo Mungu ametutendea kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa sababu ya Yesu sisi ni marafiki wa Mungu sasa.

Adamu na Kristo

12 Dhambi ilikuja ulimwenguni kwa sababu ya kile alichofanya mtu mmoja. Na dhambi ikaleta kifo. Kwa sababu hiyo ni lazima watu wote wafe, kwa kuwa watu wote wametenda dhambi. 13 Dhambi ilikuwepo ulimwenguni kabla ya Sheria ya Musa. Lakini Mungu hakutunza kumbukumbu ya dhambi ya watu wakati sheria haikuwepo. 14 Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Musa, mauti ilitawala juu ya kila mtu. Adamu alikufa kwa sababu alitenda dhambi kwa kutokutii amri ya Mungu. Lakini hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa njia hiyo hiyo walipaswa kufa.

Hivyo mtu mmoja Adamu anaweza kufananishwa na Kristo, Yeye ambaye angekuja baadaye. 15 Lakini kipawa cha Mungu hakifanani na dhambi ya Adamu. Watu wengi walikufa kwa sababu ya dhambi ya mtu huyo mmoja. Lakini neema waliyopokea watu kutoka kwa Mungu ilikuwa kuu zaidi. Wengi walikipokea kipawa cha Mungu cha uzima kwa neema ya huyu mtu mwingine, Yesu Kristo. 16 Baada ya Adamu kutenda dhambi mara moja, alihukumiwa kuwa na hatia. Lakini kipawa cha Mungu ni tofauti. Kipawa chake cha bure kilikuja baada ya dhambi nyingi, nacho kinawafanya watu wahesabiwe haki mbele za Mungu. 17 Mtu mmoja alitenda dhambi, hivyo kifo kikawatawala watu wote kwa sababu ya huyo mtu mmoja. Lakini sasa watu wengi wanaipokea neema ya Mungu iliyo nyingi sana na karama yake ya ajabu ya kufanyika wenye haki. Hakika watakuwa na uzima wa kweli na kutawala kupitia mtu mmoja, Yesu Kristo.

18 Hivyo dhambi hiyo moja ya Adamu ilileta adhabu ya kifo kwa watu wote. Lakini kwa njia hiyo hiyo, Kristo alifanya kitu chema zaidi kilichowezesha watu kufanyika wenye haki mbele za Mungu. Na hicho huwaletea uzima wa kweli. 19 Mtu mmoja hakumtiii Mungu na wengi wakafanyika wenye dhambi. Lakini kwa namna hiyo hiyo, mtu mmoja alipotii, wengi wamefanyika kuwa wenye haki. 20 Baada ya sheria kuja, zilikuwepo njia nyingi za watu kufanya makosa. Lakini kadri watu walivyozidi kufanya dhambi, ndivyo Mungu alivyomimina zaidi neema yake. 21 Hapo kale dhambi ilitumia kifo kututawala. Lakini sasa neema ya Mungu inatawala juu ya dhambi na kifo kwa sababu ya wema wake wenye uaminifu. Na hii inatuletea maisha ya milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

Footnotes

  1. 5:1 ya imani Au “uaminifu wake” au “uaminifu wa Yesu”.
  2. 5:1 sote Baadhi ya nakala muhimu za Kiyunani zina “hebu sote tuwe”.