15 Sisi tulio imara katika imani, hatuna budi kuchukuliana na udhaifu wa wale ambao si imara. Tusitafute kujipendeza wenyewe. Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake ili kumjenga katika imani. Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe bali alikuwa kama ilivyoandikwa: “Matusi yote waliyoku tukana wewe yalinipata mimi.” Kwa maana mambo hayo yaliyoan dikwa zamani, yaliandikwa kutufundisha, ili tukiwa na subira na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini. Na Mungu aliye chanzo cha subira na faraja awajalie ninyi moyo wa umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, ili kwa pamoja na kwa sauti moja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Kuhusu Umoja

Mpokeane ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowapokea, ili Mungu apate kutukuzwa. Maana nawaambia kwamba, Kristo alikuwa mtumishi kwa Waisraeli ili kuonyesha kuwa Mungu ni mwaminifu,na kuthibitisha ahadi alizowapa baba zetu. Na pia ili watu wa mataifa mengine wamtukuze Mungu kwa huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko: “Kwa sababu hii nitakutukuza kati ya watu wa mataifa, nitaimba nyimbo za kulisifu jina lako.” 10 Na tena yanasema, “Ninyi watu wa mataifa, furahini pamoja na watu wa Mungu.” 11 Na tena: “Msifuni Bwana enyi watu wote wa mataifa, watu wote wamsifu.” 12 Na tena Isaya anasema:“Shina la Yese lita chipuka, atatoka huko atakayetawala mataifa yote; na watu wa ma taifa watamtumaini.”

13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha na amani katika kumwamini, ili kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, mpate kuwa na tumaini tele.

Huduma Ya Paulo Kwa Mataifa

14 Mimi nimeridhika ndugu zangu kuwa ninyi mmejaa wema, mnao ufahamu wote, tena mnaweza kujengana. 15 Lakini kuhusu mambo fulani nimewaandikia kwa ujasiri nikiwa na shabaha ya kuwa kumbusha kwa sababu Mungu amenipa neema maalumu. 16 Amenichagua kuwa mtumishi wa Kristo Yesu kwa watu wa mataifa wasiomjua Mungu, nitoe huduma ya kikuhani kwa kuitangaza Injili ya Mungu, ili watu wa mataifa wawe sadaka inayokubaliwa na Mungu na iliy otakaswa na Roho Mtakatifu.

17 Kwa hiyo nina sababu ya kujisifu ndani ya Kristo kwa huduma yangu kwa Mungu. 18 Hata sitasema juu ya jambo lo lote isipokuwa katika yale tu ambayo Kristo mwenyewe ameyafanikisha kwa kunitumia, katika maneno na matendo yangu, akawavuta watu wa mataifa wamtii akitumia 19 nguvu za ishara na miujiza, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo kuanzia Yerusalemu mpaka kando kando ya Iliriko nimekwisha kuhubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu. 20 Shabaha yangu imekuwa nisihubiri mahali ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwin gine. 21 Lakini kama ilivyoandikwa, “Wale ambao hawajaambiwa habari zake, wataona na wale ambao hawajasikia wataelewa.”

Paulo Apanga Kwenda Roma

22 Hii ndio sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.

23 Lakini maadamu sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimetamani sana kuja kwenu, 24 natu maini kuwaona nikiwa safarini kwenda Spania, nifurahi kwa muda pamoja nanyi, kisha mnipatie msaada kwa safari hiyo. 25 Ila sasa nakwenda kupeleka msaada kwa watu wa Mungu walioko Yerusalemu. 26 Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yameamua kutoa mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu wasiojiweza walioko huko Yerusalemu. 27 Wamependa kufanya hivyo lakini kwa kweli ni wajibu wao, maana kama watu wa mataifa mengine wameshiriki katika baraka za kiroho za Waisraeli, wanawajibika kuwahudumia Waisraeli katika mahitaji yao ya kimwili. 28 Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitakwenda Spania kupitia kwenu. 29 Ninafahamu kwamba nitakapokuja kwenu, nitawaletea wingi wa baraka za Kristo.

30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo na kwa ajili ya upendo uletwao na Roho, muwe pamoja nami mkiniombea kwa Mungu. 31 Ombeni niepushwe na wale wasioamini walioko Uyahudi, na kwamba huduma yangu huko Yerusalemu ipate kukubaliwa na watu wa Mungu; 32 ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, niburudishwe pamoja nanyi. 33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amina.

15 Baadhi yetu hatuna matatizo na mambo haya. Hivyo tunapaswa kuwa wastahimilivu kwa wale wasio imara na wenye mashaka. Hatupaswi kufanya yanayotupendeza sisi bali tufanye yale yanayowapendeza wao na kwa faida yao. Tufanye chochote kinachoweza kumsaidia kila mtu kujengeka katika imani. Hata Kristo hakuishi ili kijaribu kujifurahisha yeye mwenyewe. Kama Maandiko yanavyosema, “Matusi ambayo watu waliyatoa dhidi yako pia yalinifanya niteseke.”(A) Chochote kilichoandikwa zamani kiliandikwa ili kitufundishe sisi. Maandiko haya yaliandikwa ili yatupe matumaini yanayokuja kwa njia ya subira na kutia moyo kunakoletwa nayo. Subira na kuhimiza kote hutoka kwa Mungu. Na ninawaombea ili Mungu awasaidie muwe na nia ile ile ninyi kwa ninyi, kama ilivyo nia ya Kristo Yesu. Kisha ninyi nyote, kwa sauti moja, mtamtukuza Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kristo aliwakaribisha ninyi, hivyo nanyi mkaribishane ninyi kwa ninyi. Hili litaleta heshima[a] kwa Mungu. Ndiyo, haya ndiyo maneno yangu kwenu kwamba Kristo alifanyika mtumishi wa Wayahudi ili kuonesha kuwa Mungu amefanya yale aliyowaahidi baba zao wakuu. Na pia alifanya hivi ili wale wasio Wayahudi waweze kumsifu Mungu kwa rehema anazowapa. Maandiko yanasema,

“Hivyo nitakushukuru wewe katikati ya watu wa mataifa mengine;
    Nitaliimbia sifa jina lako.”(B)

10 Na Maandiko yanasema,

“Ninyi watu wa mataifa mengine furahini pamoja na watu wa Mungu.”(C)

11 Pia Maandiko yanasema,

“Msifuni Bwana ninyi watu wote wa mataifa mengine;
    watu wote na wamsifu Bwana.”(D)

12 Na Isaya anasema,

“Mtu mmoja atakuja kutoka katika ukoo wa Yese.[b]
    Atainuka na kutawala juu ya mataifa,
na wataweka matumaini yao kwake.”(E)

13 Naomba kwamba Mungu aletaye matumaini awajaze furaha na amani kadri mnavyomwamini yeye. Na hii isababishe tumaini lenu liongezeke hadi lifurike kabisa ndani yenu kwa nguvu za Roho Mtakatifu.

Paulo Azungumzia Kazi Yake

14 Kaka na dada zangu, najua pasipo mashaka kuwa mmejaa wema na mnayo maarifa yote mnayohitaji. Hivyo kwa hakika mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi. 15 Lakini nimewaandikia ninyi kwa ujasiri wote kuhusu mambo fulani niliyotaka mkumbuke. Nilifanya hivi kwa sababu Mungu alinipa karama hii maalumu: 16 kuwa mtumishi wa Kristo Yesu kwa ajili ya wasio Wayahudi. Natumika kama kuhani ambaye kazi yake ni kuhubiri Habari Njema kutoka kwa Mungu. Alinipa mimi jukumu hili ili ninyi msio Wayahudi mweze kuwa sadaka atakayoikubali, sadaka iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.

17 Na hii ndiyo sababu najisikia vizuri kuhusu yale yote yaliyofanyika kwa ajili ya Mungu kwa kuwa mimi ni mali ya Kristo Yesu. 18 Sitazungumzia chochote nilichofanya mwenyewe. Nitazungumza tu kuhusu yale Kristo aliyofanya akinitumia mimi katika kuwaongoza wale wasiokuwa Wayahudi katika kutii. Ni yeye aliyetenda kazi katika yale niliyosema na kufanya. 19 Alitenda kazi kwa ishara za miujiza kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Matokeo yake ni kuwa nimewahubiri watu Habari Njema kuhusu Kristo kuanzia Yerusalemu na kuzunguka kote mpaka Iliriko. Na hivyo nimemaliza sehemu hiyo ya wajibu wangu. 20 Imekuwa shabaha yangu daima kuzihubiri Habari Njema katika sehemu ambako watu hawajawahi kusikia juu ya Kristo. Nafanya hivi kwa sababu sitaki kujenga katika kazi ambayo tayari mtu mwingine amekwisha kuianza. 21 Kama Maandiko yanavyosema,

“Wale ambao hawakuambiwa kuhusu yeye wataona,
    na wale ambao hawajasikia juu yake wataelewa.”(F)

Mpango wa Paulo Kwenda Rumi

22 Kazi hiyo imenifanya niwe na shughuli nyingi sana na mara nyingi imenizuia kuja kuwaona.

23 Kwa miaka mingi nimetamani kuwatembelea, na sasa nimekamilisha kazi yangu katika maeneo haya. 24 Hivyo nitawatembelea nitakapoenda Hispania. Ndiyo, napanga kusafiri kwenda Hispania na natumaini kuwatembelea nikiwa njiani. Nitakaa kwa muda na kufurahi pamoja nanyi. Kisha natumaini mtanisaidia kuendelea na safari yangu.

25 Sasa ninakwenda Yerusalemu kuwasaidia watu wa Mungu huko. 26 Baadhi yao ni maskini, na waamini kule Makedonia na Akaya walitaka kuwasaidia. Hivyo walikusanya kiasi cha fedha ili wawatumie. 27 Walifurahia kufanya hivi. Na ilikuwa kama kulipa kitu fulani walichokuwa wakidaiwa, kwa sababu kama watu wasiokuwa Wayahudi walikuwa wamebarikiwa kiroho na Wayahudi. Hivyo nao wanapaswa kutumia baraka za vitu walivyonavyo kwa ajili ya kuwasaidia Wayahudi. 28 Naelekea Yerusalemu kuhakikisha kuwa maskini wanapokea fedha hizi zilizotolewa kwa ajili yao.

Nitakapokuwa nimekamilisha hilo, nitaondoka kuelekea Hispania na nikiwa njiani nitasimama ili niwaone. 29 Na ninajua kwamba nitakapowatembelea, nitakuja na baraka zote anazotoa Kristo.

30 Kaka na dada zangu, nawaomba mnisaidie katika kazi hii kwa kuniombea kwa Mungu. Fanyeni hivi kwa sababu ya Bwana wetu Yesu Kristo na pendo ambalo Roho anatupa. 31 Niombeeni ili niokolewe kutokana na wale walioko Yudea wanaokataa kuupokea ujumbe wetu. Pia ombeni kwamba msaada huu ninaoupeleka Yerusalemu utakubalika kwa watu wa Mungu huko. 32 Kisha, nitakuwa na furaha wakati nitakapokuja kuwaona, Mungu akipenda. Na ndipo tutaweza kufurahia muda wa kujengana sisi kwa sisi. 33 Mungu anayetoa amani awe pamoja nanyi nyote. Amina.

Footnotes

  1. 15:7 heshima Au “utukufu”. Tazama Utukufu katika Orodha ya Maneno.
  2. 15:12 ukoo wa Yese Yese alikuwa baba wa Daudi, mfalme wa Israeli. Yesu alizaliwa katika ukoo huu.