Kutii Mamlaka

13 Kila mtu hana budi kutii serikali inayotawala. Kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na serikali zote zilizopo zimewekwa na Mungu. Kwa hiyo anayepinga mamlaka inayotawala ana pinga chombo kilichowekwa na Mungu; na watu wanaoasi watajiletea hukumu. Kwa maana watawala hawatishi watu wanaotenda mema bali wale wanaotenda maovu. Kama hupendi kuishi kwa kumwogopa mwenye mamlaka, basi tenda mema naye atakusifu. Maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa manufaa yako. Lakini kama ukitenda maovu, basi ogopa kwa maana hatembei na silaha bure. Yeye ni mtumishi wa Mungu anayetekeleza adhabu ya Mungu juu ya watenda maovu. Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu tu bali pia kwa ajili ya dhamiri.

Kwa sababu hiyo hiyo mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu ambao hutumia muda wao wote kutawala. Wal ipeni wote haki zao; mtu wakodi mlipe kodi; na mtoza ushuru mli pe ushuru; astahilie kunyenyekewa, mnyenyekee; astahiliye hesh ima, mheshimu.

Upendo Na Sheria

Msiwe na deni la mtu ye yote; isipokuwa deni la kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria. Kwa maana amri zisemazo: Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 10 Upendo haumfanyii jirani jambo baya, kwa hiyo upendo unakamilisha sheria zote.

11 Fanyeni hivi mkitambua kuwa sasa tumo katika wakati gani. Huu ni wakati wa kuamka kutoka usingizini, kwa maana wokovu wetu umekaribia zaidi sasa kuliko wakati tulipoamini kwa mara ya kwanza. 12 Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Kwa hiyo tutupe kando matendo ya giza, tuvae silaha za nuru. 13 Tuishi maisha ya heshima kama inavyopasa wakati wamchana: si kwa ulafi na ulevi; si kwa ufisadi na uasherati; si kwa ugomvi na wivu. 14 Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, na msitoe nafasi kwa miili yenu yenye asili ya dhambi, kutimiza tamaa zake.

Kutii Watawala

13 Watiini watawala wa serikali. Hakuna anayeweza kutawala bila mamlaka ya Mungu. Mamlaka ya kutawala hutoka kwa Mungu. Hivyo yeyote anayekuwa kinyume na serikali hakika anakuwa kinyume na kitu ambacho Mungu amekiweka. Wale walio kinyume na serikali wanajiletea adhabu wao wenyewe. Watu wanaotenda mema hawawaogopi watawala. Bali wale wanaotenda mabaya ni lazima wawaogope watawala. Je, mnataka kuwa huru mbali na kuwaogopa hao? Basi mfanye yaliyo sahihi tu, nao watawasifu ninyi.

Watawala ni watumishi wa Mungu kwa ajili ya kuwasaidia ninyi. Lakini mkifanya yasiyo sahihi, mnayo sababu ya kuwa na woga. Hao wanayo mamlaka ya kuwaadhibu, na watayatumia mamlaka hayo. Wao ni watumishi wa Mungu ili wawaadhibu wale wanaofanya yale yasiyo sahihi. Kwa hiyo mnapaswa kuitii serikali, siyo tu kwa sababu mtaadhibiwa, bali kwa sababu mnajua kuwa ni jambo lililo sahihi kufanya hivyo.

Na hii ndiyo sababu mnalipa kodi. Watawala hawa wanapaswa kulipwa kwa ajili ya kutimiza wajibu wao wote walionao wa kutawala. Hakika wanatumika kwa ajili ya Mungu. Wapeni watu wote vile wanavyowadai. Kama wanawadai aina yoyote ya kodi, basi lipeni. Onesheni heshima kwa wale mnaopaswa kuwaheshimu. Na onesheni uadilifu kwa wale mnaopaswa kuwafanyia hivyo.

Kuwapenda Wengine Ndiyo Sheria Pekee

Msidaiwe chochote na mtu, isipokuwa mdaiwe upendo baina yenu. Mtu anayewapenda wengine anakuwa amefanya yote yanayoamriwa na sheria. Sheria inasema, “Usizini, usiue, usiibe, usitamani kitu cha mtu mwingine.”(A) Amri hizo zote na zingine hakika zinajumlishwa na kuwa kanuni moja tu, “Mpende jirani yako[a] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.”(B) 10 Upendo hauwaumizi wengine. Hivyo kupenda ni sawa na kuitii sheria yote.

11 Nalisema hili kwa sababu mnajua kwamba tunaishi katika wakati ulio muhimu. Ndiyo, ni wakati wenu sasa kuamka kutoka usingizini. Wokovu wetu sasa uko karibu zaidi kuliko ilivyokuwa tulipoamini kwa mara ya kwanza. 12 Usiku karibu umekwisha. Na mchana karibu unaingia. Hivyo tunapaswa kuacha kufanya chochote kinachohusiana na giza. Tunapaswa kujiandaa kuupiga uovu kwa silaha za nuru. 13 Tunapaswa kuishi katika njia sahihi, kama watu walio wa mchana. Hatupaswi kuwa na tafrija za ovyo ama kulewa. Hatupaswi kujihusisha katika dhambi ya uzinzi au ya aina yoyote ya mwenendo usiofaa. Hatupaswi kusababisha mabishano au kuwa na wivu. 14 Bali, muwe kama Kristo Yesu katika kila jambo mnalolitenda,[b] ili watu watakapowaangalia, waweze kumwona yeye. Msifikirie namna ya kuridhisha matakwa ya udhaifu wa mwanadamu na tamaa zake.

Footnotes

  1. 13:9 jirani yako Au “wengine”. Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
  2. 13:14 Bali, muwe … jambo mnalolitenda Kwa maana ya kawaida, “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo.”