Njia Ya Kweli Ya Wokovu

Hatimaye ndugu zangu, furahini katika Bwana. Mimi sichoki kuwaandikieni mambo yale yale niliyokwisha waandikia kwa maana najua kwamba yatakuwa ni kinga kwenu. Jihadharini na watenda maovu, hao mbwa, na wale wanaokaza mafundisho ya kutahiriwa. Sisi tumepokea tohara ya kweli, kwa maana tunamwabudu Mungu katika Roho. Sisi tunaona fahari kwa ajili ya maisha yetu ndani ya Kristo Yesu. Hatuweki matumaini yetu katika mambo ya mwili, ijapokuwa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuweka matumaini katika mambo hayo. Kama mtu mwingine ye yote anadhani kuwa anazo sababu za kuweka matumaini yake katika mambo ya mwili, basi mimi ninazo sababu zaidi. Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwis raeli wa kabila la Benjamini; Mwebrania halisi. Kuhusu mambo ya kushika sheria, mimi nilikuwa Mfarisayo; na kwa upande wa juhudi, mimi nilikuwa na bidii katika kutesa kanisa; na kuhusu haki ipatikanayo kwa kutii sheria, mimi nilikuwa sina hatia.

Lakini mambo hayo niliyoyaona mwanzo kuwa ni faida kwangu, sasa nayaona kuwa ni hasara kwa ajili ya Kristo. Zaidi ya hayo, nahesabu mambo yote kuwa hasara tupu yakilinganishwa na faida kubwa ninayopata kwa kumjua Kristo Yesu aliye Bwana wangu. Kwa ajili yake nilikubali kupoteza kila kitu na kuona mambo hayo yote kuwa ni takataka ili nipate faida ya kuwa na Kristo; na nikiwa kwake nisionekane kama mtu mwenye haki yake mwenyewe, inayotokana na kushika sheria, bali niwe na ile haki inayotokana na kumwamini Kristo, ambaye yeye ni haki itokayo kwa Mungu inayopatikana kwa imani. 10 Nataka nimjue Kristo na nguvu ya ufufuo wake na nishi riki mateso yake, niwe kama yeye katika kifo chake; 11 na hivyo, kama ikiwezekana, niufikie ufufuo kutoka kwa wafu.

12 Sisemi kwamba nimekwisha kupokea haya yote, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha; bali nazidi kukaza mwendo ili nipate kile ambacho, kwa ajili yake, Kristo amenifanya niwe wake. 13 Ndugu zangu, bado sijihesabu kuwa nimekwisha pata ile zawadi. Lakini jambo moja ninalofanya ni kusahau mambo yote yali yopita, na kukaza mwendo kufikia yaliyo mbele yangu. 14 Nakaza na nifikie ushindi, ili nipate zawadi ambayo Mungu ameniitia mbinguni, nikiwa ndani ya Kristo Yesu.

15 Sisi tuliokomaa kiroho tuwe na msimamo kama huu. Lakini kama kuna mawazo tofauti kuhusu jambo lo lote, Mungu atawafunu lia. 16 Ila tushike sana yale tuliyokwisha kupokea.

17 Ndugu zangu, nawasihi mfuate mfano wangu, na muwatazame wale wanaofuata mfano tuliowapa. 18 Kwa maana, kama nilivyok wisha waambia kabla, na sasa nasema tena kwa machozi, wako watu wengi miongoni mwenu ambao maisha yao yanaonyesha kuwa wao ni adui wa msalaba wa Kristo. 19 Mwisho wa watu hao ni kuangamia, na Mungu wao ni tumbo; kwa sababu wao huyaonea fahari mambo ya aibu na mawazo yao yametawaliwa na mambo ya dunia. 20 Lakini uraia wetu uko mbinguni. Nasi tunangoja kwa hamu Mwokozi kutoka huko, yaani Bwana wetu Yesu Kristo, 21 ambaye, kwa uwezo unaomwezesha kutawala kila kitu, atabadilisha miili yetu midhaifu ili iwe na utukufu kama alionao yeye.

Yesu Kristo ni wa Muhimu Zaidi

Kwa hiyo sasa, kaka na dada zangu, furahini kwa kuwa ninyi ni wa Bwana. Sisiti kuwaandikia mambo haya haya, kwa sababu yatawasaidia ninyi kuwa imara na salama.

Mjihadhari na mbwa, mjihadhari na wafanyakazi waovu, mjihadhari na watu wanaotaka kumkata kila mtu ambaye hajatahiriwa.[a] Lakini sisi ndiyo wenye tohara[b] ya kweli, tunaomwabudu Mungu kupitia Roho wake. Hatutumaini katika namna tulivyo kwa kuzaliwa au kwa yale tuliyoyakamilisha. Tunajivuna kuwa sisi ni milki ya Kristo Yesu. Hata kama ninaweza kujitumainisha mimi mwenyewe, bado sifanyi hivyo. Ikiwa kuna watu wanadhani wana sababu za kutumaini sifa za kibinadamu, wanapaswa kujua kuwa nina sababu zaidi za kufanya hivyo. Nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa. Mimi ni Myahudi wa kabila la Benjamini. Mimi ni Mwebrania halisi, hata wazazi wangu pia. Nikawa Farisayo na nilitii torati kwa uangalifu sana. Nilikuwa na hamu sana ya kumridhisha Mungu[c] hata nikalitesa kanisa. Kwa usahihi niliitii sheria ya Musa.

Wakati fulani mambo haya yote yalikuwa muhimu kwangu. Lakini kwa sababu ya Kristo, sasa ninayachukulia mambo haya yote kuwa yasiyo na thamani. Na si haya tu, lakini sasa ninaelewa kuwa kila kitu ni hasara tu ukilinganisha na thamani kuu zaidi ya kumjua Kristo Yesu, ambaye sasa ni Bwana wangu. Kwa ajili yake nilipoteza kila kitu. Na ninayachukulia yote kama kinyesi, ili nimpate Kristo. Ninataka niwe wake. Katika Kristo ninayo haki mbele za Mungu, lakini kuwa na haki mbele za Mungu hakuji kwa kuitii sheria, Bali inakuja toka kwa Mungu kupitia imani kwa[d] Kristo. Mungu anatumia imani yangu kwa Kristo kunihesabia haki. 10 Ninachotaka ni kumjua Kristo na nguvu iliyomfufua kutoka kwa wafu. Ninataka kushiriki katika mateso yake na kuwa kama yeye hata katika kifo chake. 11 Kisha mimi mwenyewe naweza kuwa na matumaini kwamba nitafufuliwa kutoka kwa wafu.

Kuyafikia Malengo

12 Sisemi kuwa nimekwisha kupata ujuzi huo au kuifikia shabaha ya mwisho. Lakini bado ninajitahidi kuifikia shabaha kwa kuwa ndivyo ambavyo Kristo Yesu anataka nifanye. Ndiyo sababu alinifanya kuwa wake. 13 Kaka na dada zangu, ninajua ya kuwa bado nina safari ndefu. Lakini kuna kitu kimoja ninachofanya, nacho ni kusahau yaliyopita na kujitahidi kwa kadri ninavyoweza kuyafikia malengo yaliyo mbele yangu. 14 Ninaendelea kupiga mbio kuelekea mwisho wa mashindano ili niweze kushinda tuzo ambayo Mungu ameniitia kutoka mbinguni kwa njia ya Kristo Yesu.

15 Sisi sote tuliokua kiroho tunapaswa kufikiri namna hii. Na ikiwa kuna jambo lolote ambalo hamkubaliani nalo, Mungu atalifunua kwenu. 16 Lakini tunapaswa kuendelea kuifuata kweli tuliyonayo tayari.

17 Kaka na dada zangu, unganeni pamoja na mfuate mfano wangu. Mtazame na mjifunze pia kutoka kwa wale wanaoishi katika namna tuliyoionesha kwenu. 18 Wapo wengi ambao mwenendo wao unaonesha kuwa ni adui za msalaba wa Kristo. Nimekwishawaambia kuhusu hao mara nyingi. Na inanifanya nitokwe machozi ninapowaambia kuhusu watu hao sasa. 19 Wanauendea uharibifu kwa namna wanavyoishi. Wanaabudu tamaa za mili yao kana kwamba hizo ndizo Mungu. Wanatenda mambo ya aibu na wanajivuna kwa kutenda mambo hayo. Wanayawazia mambo ya kidunia tu. 20 Lakini sisi tunatawaliwa na serikali iliyoko mbinguni. Tunamsubiri Mwokozi wetu, Bwana wetu Yesu Kristo atakayekuja kutoka mbinguni. 21 Ataibadilisha miili yetu minyenyekevu na kuifanya iwe kama mwili wake yeye mwenyewe, mwili wenye utukufu. Kristo atafanya hivi kwa nguvu yake inayomwezesha kutawala juu ya vyote.

Footnotes

  1. 3:2 wanaotaka … hajatahiriwa Neno la msingi hapa ni kama “tohara” (tazama Tahiri, kutahiriwa, tohara katika Orodha ya Maneno), Lakini hapa inamaanisha “kukata kiungo cha mwili” au “kukatakata vipande”.
  2. 3:3 tohara Neno hili limetumika hapa kumaanisha hali ya kiroho. Tazama Tahiri, kutahiriwa, tohara katika Orodha ya Maneno.
  3. 3:6 hamu sana ya kumridhisha Mungu Kabla Paulo hajawa mwamini katika Yesu kama Mfalme Aliyeteuliwa na Mungu, alidhani kuwa alikuwa na wajibu kama Farisayo mwema wa kuwapinga Wayahudi waliokuwa wafuasi wa Kristo.
  4. 3:9 imani kwa Au, “uaminifu wa”.