Add parallel Print Page Options

Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao

(Mk 13:1-31; Lk 21:5-33)

24 Yesu alipokuwa anaondoka eneo la Hekalu, wanafunzi wake walimwendea na kumwonyesha majengo ya Hekalu. Akawauliza, “Mnayaona majengo haya? Ukweli ni kuwa, yataharibiwa. Kila jiwe litadondoshwa chini, hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe jingine.”

Baadaye, Yesu alipokuwa ameketi mahali fulani katika Mlima wa Mizeituni, Wafuasi wake walimwendea faraghani. Wakasema, “Twambie mambo haya yatatokea lini. Na nini kitatokea ili kutuandaa kwa ajili ya ujio wako na mwisho wa nyakati?”

Yesu akajibu, “Mjihadhari! Msimruhusu mtu yeyote awadanganye. Watu wengi watakuja na watatumia jina langu. Watasema, ‘Mimi ndiye Masihi.’ Na watawadanganya watu wengi. Mtasikia kuhusu vita vinanavyopiganwa na pia matetesi ya kuwapo vita vingine. Lakini msiogope. Mambo haya lazima yatokee na mwisho wenyewe hautafuata palepale. Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. Utakuwepo wakati wa njaa ambapo watu watakosa chakula. Na kutakuwa matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Mambo haya ni mwanzo wa matatizo, kama uchungu wa kwanza mwanamke anapozaa.

Kisha mtakamatwa na kupelekwa kwa wenye mamlaka ili mhukumiwe na kuuawa. Watu wote katika ulimwengu watawachukia kwa sababu mnaniamini mimi. 10 Nyakati hizo watu wengi wataacha kuwa wafuasi wangu. Watasalitiana na kuchukiana. 11 Manabii wengi watatokea na kusababisha watu wengi kuamini mambo yasiyo ya kweli. 12 Kutakuwepo na uovu mwingi sana duniani kiasi kwamba upendo wa waaminio wengi utapoa. 13 Lakini yeyote yule atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 14 Na Habari Njema niliyoihubiri kuhusu Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote. Itatawanywa katika kila taifa. Kisha mwisho utakuja.

15 Nabii Danieli alizungumza kuhusu ‘jambo la kutisha litakalosababisha uharibifu.’[a] Mtakapoliona jambo hili la kutisha limesimama patakatifu.” (Asomaye hili anapaswa kuelewa jambo hili linamaanisha nini.) 16 “Watu walio Uyahudi wakimbilie milimani. 17 Wakimbie pasipo kupoteza muda ili kuchukua kitu chochote. Wakiwa darini wasiteremke ili kuchukua kitu na kukitoa nje ya nyumba. 18 Wakiwa shambani wasirudi nyumbani kuchukua koti.

19 Itakuwa hali ngumu kwa wanawake wenye mimba na wenye watoto wachanga! 20 Ombeni isiwe majira ya baridi au isiwe siku ya Sabato mambo haya yatakapotokea na mkalazimika kukimbia, 21 kwa sababu utakuwa wakati wa dhiki kuu. Kutakuwepo na usumbufu mwingi sana kuliko ule uliowahi kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu. Na hakuna jambo baya kama hilo litakalotokea tena.

22 Lakini Mungu amekwisha amua kuufupisha wakati huo. Ikiwa usingefupishwa, hakuna ambaye angeendelea kuishi. Lakini Mungu ataufupisha ili kuwasaidia watu aliowachagua.

23 Wakati huo watu wataweza kuwaambia, ‘Tazama, Masihi yuko kule!’ Au wakasema, ‘Ni yule!’ Msiwaamini. 24 Manabii wa uongo na masihi wa uongo watatokea na kufanya miujiza na maajabu[b] makuu, ili ikiwezekana wawadanganye wateule. 25 Na sasa nimewatahadharisha kuhusu hili kabla halijatokea.

Read full chapter

Footnotes

  1. 24:15 jambo … uharibifu Tazama Dan 9:27; 12:11 (pia Dan 11:31).
  2. 24:24 miujiza na maajabu Hapa ina maana ya kazi za ajabu zinazofanywa kwa kutumia nguvu za Shetani.