Waamini Wa Efeso Wapokea Roho Mtakatifu

19 Wakati Apolo alikuwa Korintho, Paulo alipitia sehemu za kaskazini akafika Efeso. Huko aliwakuta wanafunzi kadhaa, aka wauliza, “Mlipoamini mlipokea Roho Mtakatifu?” Wakajibu, “Hapana. Hatujawahi hata kusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.” Ndipo Paulo akawauliza, “Mlibatizwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Ubatizo wa Yohana.” Paulo akasema, “Yohana alipobatiza, aliwaambia watu watubu dhambi na kumwamini atakayekuja baada yake, yaani, Yesu.” Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Yesu. Na Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia , wakasema kwa lugha mpya na kutabiri. Walikuwepo kama watu kumi na wawili.

Paulo akaingia katika sinagogi na kwa muda wa miezi mitatu akafundisha kwa ujasiri akitumia kila njia kueleza juu ya Ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao walipokataa kuamini na kuanza kukashifu ujumbe wake mbele ya ushirika wote, aliachana nao, akawachukua wale wanafunzi akaendelea kujadiliana nao katika ukumbi wa Tirano. 10 Aliendelea na kazi hii kwa muda wa miaka miwili mpaka wenyeji wote wa Asia wakawa wamesikia neno la Bwana,

Wana Wa Skeva Wajaribu Kutoa Pepo

11 Na Mungu alifanya miujiza mingi ya ajabu kwa mkono wa Paulo. 12 Watu wakachukua vitambaa na taulo ambazo zilikuwa zimegusa mwili wa Paulo wakawawekea wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao na pepo wachafu wakawatoka. 13 Baadhi ya Wayahudi waliokuwa wakienda huku na huko wakiwatoa watu pepo wachafu wali jaribu nao kutumia jina la Yesu kutoa pepo, wakisema, “Nakuamuru kwa jina la Yesu, anayehubiriwa na Paulo.” 14 Palikuwa na wana saba wa kuhani mkuu aliyeitwa Skeva ambao walikuwa wakifanya hivi. 15 Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namfahamu na Paulo pia namfahamu; lakini ninyi ni nani?” 16 Yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia akawashambulia vikali, wakatoka ndani ya ile nyumba mbio wakiwa uchi na wenye majeraha. 17 Jambo hili likajulikana kwa wenyeji wote wa Efeso, Wayahudi kwa Wagiriki; hofu ikawajaa watu wote; na jina la Bwana likaheshimiwa. 18 Waamini wengi wakatubu matendo yao maovu hadharani. 19 Na wale waliokuwa wakishiriki uchawi na kupiga ramli wakaleta vitabu vyao na kuvichoma moto hadharani. Walipopiga hesabu ya vitabu walivyochoma walikuta kwamba thamani yake ilikuwa vipande elfu hamsini vya fedha. 20 Neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu.

Ghasia Huko Efeso

21 Baada ya mambo haya kutokea, Paulo aliongozwa na Roho kupitia Makedonia na Akaya akiwa njiani kwenda Yerusalemu. Paulo alisema, “Nikishafika Yerusalemu, ni lazima niende Rumi pia.” 22 Akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, naye akakaa Asia kwa muda kidogo zaidi. 23 Wakati huo huo pakatokea ghasia kubwa kwa sababu ya Njia ya Bwana. 24 Mtu mmoja aitwaye Demetrio mhunzi wa vinyago vya fedha alikuwa akitengeneza vihekalu vya fedha vya Artemi na kuwa patia mafundi wake biashara kubwa. 25 Yeye aliwakutanisha watu hawa pamoja na watu wengine wanaofanya kazi za kutengeneza viny ago vya miungu kama wao akawaambia, “Jamani, mnajua ya kuwa uta jiri wetu unatokana na kazi zetu. 26 Lakini mmeona na kusikia jinsi ambavyo huko Efeso na karibu Asia yote huyu Paulo amewash awishi watu na kutuharibia biashara kwa kusema kuwa miungu iliy otengenezwa na watu si miungu ya kweli. 27 Kwa hiyo kuna hatari kuwa kazi yetu itaanza kudharauliwa. Na si hivyo tu, bali hata hekalu la mungu wetu Artemi, aliye mkuu na anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa halina maana tena na utukufu wake utaondolewa.”

28 Waliposikia maneno haya walighadhabika wakapiga kelele, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!” 29 Mji mzima ukajaa vurugu, waka kimbilia katika ukumbi wa michezo kwa pamoja wakawakamata Gayo na Aristarko, Wamakedonia waliokuwa wakisafiri na Paulo. 30 Paulo alitaka kuingilia kati lakini wanafunzi wengine wakam zuia; 31 hata baadhi ya viongozi waliokuwa marafiki wa Paulo walituma watu wamsihi asiingie katika ule ukumbi. 32 Pakawa na kutokuelewana katika ule ukumbi kwa sababu baadhi ya watu wali kuwa wakisema jambo moja na wengine lingine. Ikawa ni fujo; wengi wa watu waliofika hawakujua ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko. 33 Wayahudi wakamchagua Aleksanda azungumze kwa niaba yao naye akawaashiria watu wanyamaze apate kuzungumza. 34 Lakini umati ulipogundua yakuwa yeye ni Myahudi, walipiga kelele kwa kiasi cha saa mbili wakisema, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!” 35 Baadaye karani wa mji alipofanikiwa kuwanyamazisha, aliwahu tubia akasema, “Ndugu Waefeso, kila mtu ulimwenguni anajua ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu iliyoanguka kutoka angani. 36 Kwa hiyo, kwa kuwa hakuna anayeweza kukanusha mambo haya, sioni sababu ya ninyi kufanya fujo au kuchukua hatua ambazo baadaye huenda mkazijutia. 37 Kwa maana mmewaleta hawa watu wawili hapa ingawa wao hawaja fanya uharibifu wo wote kwa hekalu la Artemi au kusema maneno ya kufuru juu ya huyu mungu wetu mwanamke. 38 Kama Demetrio na mafundi wenzake wana mashtaka juu ya mtu ye yote, mahakama ziko wazi na mahakimu wapo; wachukue hatua za kisheria. 39 Lakini kama kuna mashauri mengine, itabidi mtumie baraza halali. 40 Hivi sasa tuko katika hatari ya kushtakiwa kwa kufanya fujo kwa maana hatuna sababu ya kuridhisha kuhusu mambo yaliyotokea leo.” 41 Baada ya kusema haya akavunja mkutano.

Paulo Akiwa Efeso

19 Apolo alipokuwa katika mji wa Korintho, Paulo alikuwa anatembelea baadhi ya sehemu akiwa njiani kwenda Efeso. Alipofika Efeso waliwakuta baadhi ya wafuasi wa Bwana. Akawauliza, “Mlimpokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”

Wafuasi hao wakamwambia, “Hatujawahi hata kusikia kuhusu Roho Mtakatifu!”

Paulo akawauliza, “Kwa hiyo ni mlibatizwa kwa ubatizo gani?”

Wakasema, “Kwa ubatizo aliofundisha Yohana.”

Paulo akasema, “Yohana aliwaambia watu wabatizwe kuonesha kuwa walidhamiria kubadili maisha yao. Aliwaambia watu kuamini katika yule atakaye kuja baada yake, naye huyo ni Yesu.”

Wafuasi hawa waliposikia hili, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. Kisha Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akaja juu yao. Wakaanza kuzungumza na kutabiri katika lugha tofauti. Walikuwepo wanaume kama kumi na mbili katika kundi hili.

Paulo akaingia katika sinagogi na akazungumza kwa ujasiri. Aliendelea kufanya hivi kwa miezi mitatu. Alizungumza na Wayahudi, akijaribu kuwashawishi kukubali alichokuwa anawaambia kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao wakawa wakaidi, wakakataa kuamini. Waliikashifu Njia[a] ya Bwana mbele ya kila mtu. Hivyo Paulo aliwaacha Wayahudi hawa na kuwachukua wafuasi wa Bwana pamoja naye. Alikwenda mahali ambapo mtu aitwaye Tirano alikuwa na shule. Hapo Paulo alizungumza na watu kila siku. 10 Alifanya hivi kwa miaka miwili na kila mtu aliyeishi Asia, Wayahudi na Wayunani alilisikia neno la Bwana.

Wana wa Skewa

11 Mungu alimtumia Paulo kufanya miujiza ya kipekee. 12 Baadhi ya watu walichukua vitambaa vya mkononi na nguo zilizovaliwa na Paulo na kuziweka juu ya wagonjwa. Wagonjwa waliponywa na pepo wabaya waliwatoka watu.

13-14 Pia baadhi ya Wayahudi walikuwa wanasafiri huku na huko wakiwatoa pepo wabaya kwa watu. Wana saba wa Skewa, mmoja wa viongozi wa makuhani, walikuwa wakifanya hili. Wayahudi hawa walijaribu kutumia jina la Bwana kuyatoa mapepo kwa watu. Wote walikuwa wanasema, “Katika jina la Bwana Yesu anayezungumzwa na Paulo ninakuamuru utoke!”

15 Lakini wakati fulani pepo akawaambia Wayahudi hawa, “Ninamfahamu Yesu, na ninafahamu kuhusu Paulo, na ninyi ni nani?”

16 Kisha mtu aliyekuwa na pepo ndani yake akawarukia. Alikuwa na nguvu kuliko wote. Akawapiga, akawachania nguo za na kuwavua, nao wakakimbia kutoka katika nyumba ile wakiwa uchi.

17 Watu wote katika Efeso, Wayahudi na Wayunani wakafahamu kuhusu hili. Wakaogopa na kumtukuza Bwana Yesu. 18 Waamini wengi walianza kukiri, wakisema mambo yote maovu waliyotenda. 19 Baadhi yao walikuwa wametumia uchawi huko nyuma. Waamini hawa walileta vitabu vyao vya uchawi na kuvichoma mbele ya kila mtu. Vitabu hivi vilikuwa na thamani ya sarafu hamsini elfu za fedha.[b] 20 Hivi ndivyo ambavyo neno la Bwana lilikuwa linasambaa kwa nguvu, likisababisha watu wengi kuamini.

Paulo Apanga Safari

21 Baada ya hili, Paulo alipanga kwenda Yerusalemu. Alipanga kupitia katika majimbo ya Makedonia na Akaya kisha kwenda Yerusalemu. Alisema, “Baada ya kwenda Yerusalemu, ni lazima niende Rumi pia.” 22 Timotheo na Erasto walikuwa wasaidizi wake wawili. Paulo aliwatuma watangulie Makedonia. Lakini yeye alikaa Asia kwa muda.

Tatizo Katika Mji wa Efeso

23 Lakini katika wakati huo huo kulikuwepo tatizo kuhusiana na Njia. Hivi ndivyo ilivyotokea: 24 Alikuwepo mtu aliyeitwa Demetrio aliyekuwa mfua fedha. Alikuwa akitengeneza sanamu ndogo za fedha zilizofanana na hekalu la Artemi, mungu mke. Wanaume waliokuwa wakifanya kazi hii walijipatia pesa nyingi sana.

25 Demetrio alifanya mkutano na watu hawa pamoja na wengine waliokuwa wanafanya kazi ya aina hiyo. Akawaambia, “Ndugu, mnafahamu kuwa tunapata pesa nyingi kutokana na kazi yetu. 26 Lakini angalieni kitu ambacho mtu huyu Paulo anafanya. Sikilizeni anachosema. Amewashawishi watu wengi katika Efeso na karibu Asia yote kubadili dini zao. Anasema miungu ambayo watu wanatengeneza kwa mikono si miungu wa kweli. 27 Ninaogopa hili litawafanya watu kuwa kinyume na biashara yetu. Lakini kuna tatizo jingine pia. Watu wataanza kufikiri kuwa hekalu la Artemi, mungu wetu mkuu halina maana. Ukuu wake utaharibiwa. Na Artemi ni mungu mke anayeabudiwa na kila mtu katika Asia na ulimwengu wote.”

28 Waliposikia hili, walikasirika sana. Wakapaza sauti zao wakisema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!” 29 Mji wote ukalipuka kwa vurugu. Watu wakawakamata Gayo na Aristarko, waliotoka Makedonia waliokuwa wanasafiri na Paulo, wakawapeleka kwenye uwanja wa mji. 30 Paulo alitaka kwenda ili azungumze na watu, lakini wafuasi wa Bwana walimzuia. 31 Pia, baadhi ya viongozi katika jimbo la Asia waliokuwa rafiki zake walimtumia ujumbe wakimwambia asiende uwanjani.

32 Watu wengi walikuwa akipiga kelele kusema hili na wengine walisema jambo jingine. Mkutano ukawa na vurugu kubwa. Watu wengi hawakujua ni kwa nini walikwenda pale. 33 Baadhi ya Wayahudi wakamshawishi mtu mmoja aliyeitwa Iskanda asimame mbele ya umati, wakamwelekeza cha kusema. Iskanda alipunga mkono wake, akijaribu kuwaeleza watu jambo. 34 Lakini watu walipoona kuwa Iskanda ni Myahudi, wote wakaanza kupiga kelele ya aina moja. Kwa masaa mawili waliendelea kusema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!”

35 Ndipo karani wa mji akawashawishi watu kunyamaza. Akawaambia, “Watu wa Efeso, kila mtu anafahamu kwamba Efeso ndiyo mji unaotunza hekalu la mungu mkuu mke Artemi. Kila mtu anafahamu pia kwamba tunatunza mwamba wake mtakatifu.[c] 36 Hakuna anayeweza kupinga hili, hivyo mnyamaze. Ni lazima mtulie na kufikiri kabla hamjafanya kitu chochote.

37 Mmewaleta watu[d] hawa hapa, lakini hawajasema kitu chochote kibaya kinyume na mungu wetu mke. Hawajaiba kitu chochote kutoka kwenye hekalu lake. 38 Tuna mahakama za sheria na wapo waamuzi. Je, Demetrio na watu hawa wanaofanya kazi pamoja naye wana mashitaka dhidi ya yeyote? Wanapaswa kwenda mahakamani wakawashtaki huko.

39 Kuna kitu kingine mnataka kuzungumzia? Basi njooni kwenye mikutano ya kawaida ya mji mbele ya watu. Litaweza kuamuriwa huko. 40 Ninasema hivi kwa sababu mtu mwingine anaweza kuona tukio hili la leo na akatushtaki kwa kuanzisha ghasia. Hatutaweza kufafanua vurugu hii, kwa sababu hakuna sababu za msingi za kuwepo mkutano huu.” 41 Baada ya karani wa mji kusema hili, aliwaambia watu kwenda majumbani mwao.

Footnotes

  1. 19:9 Njia Au “Njia ya Bwana”. Tazama pia katika Mdo 9:2; 18:25-26; 19:23; 22:4,22.
  2. 19:19 sarafu hamsini elfu za fedha Kila sarafu, Sarafu ya Kiyunani iliyoitwa drachma ilikuwa na thamani ya ujira au mshahara wa siku moja.
  3. 19:35 mwamba wake mtakatifu Pengine kilikuwa kimondo au mwamba au jiwe ambalo watu walidhani linafanana na Artemi na hivyo waliliabudu.
  4. 19:37 watu Gayo na Aristarko, waliokuwa wanasafiri na Paulo.