Yesu Awashutumu Walimu Wa Sheria Na Mafarisayo

23 Kisha Yesu akawaambia ule umati wa watu pamoja na wana funzi wake: “Walimu wa sheria na Mafarisayo wamechukua nafasi ya Musa, kwa hiyo watiini na kufanya yote wanayowaambia mfa nye. Lakini msifuate matendo yao; kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri. Wao hufunga mizigo mikubwa na kuwabebesha watu, lakini wao wenyewe hawajaribu hata kunyoosha kidole kuisogeza!

“Wao hufanya mambo yao yote ili waonekane na watu. Wanavaa vipande vipana vya ngozi vilivyoandikwa sheria na kurefusha zaidi pindo za mavazi yao ya sala. Wanapenda kukaa viti vya wageni wa heshima karamuni na viti vya mbele katika masinagogi. Hupenda kuamkiwa masokoni na kuitwa ‘Rabi.’

“Lakini ninyi msipende kuitwa ‘Rabi’ kwa sababu mnaye rabi mmoja, na ninyi nyote ni ndugu. Na msimwite mtu ye yote hapa duniani ‘baba’ kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni. 10 Hali kadhalika msipende kuitwa ‘mabwana’ kwa maana mnaye Bwana mmoja tu, yaani Kristo. 11 Aliye mkuu kuliko ninyi nyote atakuwa mtumishi wenu. 12 Ye yote anayejikuza atashushwa; na ye yote anayejinyenyekeza atainuliwa.

13 “Lakini ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnafungia watu milango ya Ufalme wa mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, wala hamruhusu wale ambao wange penda kuingia waingie. [

14 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wana fiki! Mnadhulumu nyumba za wajane, na kwa kujionyesha kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo adhabu yenu itakuwa kubwa zaidi.”]

15 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wana fiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja awe mfuasi wa dini yenu, lakini baada ya kumpata, mnamfanya astahili kwenda Jehena mara mbili zaidi yenu!

16 “Ole wenu viongozi vipofu! Ninyi mnasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini mtu akiapa kwa dhahabu iliyoko Hekaluni, itambidi atimize kiapo hicho.’ 17 Ninyi vipofu wajinga! Ni kipi kilicho bora zaidi, ni ile dhahabu au ni Hekalu ambalo ndilo linafanya dhahabu hiyo kuwa takatifu? 18 Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu, lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyoko madhabahuni itambidi atimize kiapo hicho.’ 19 Ninyi vipofu! Ni kipi bora zaidi, sadaka, au madhabahu ambayo ndio inafanya sadaka hiyo kuwa takatifu? 20 Kwa hiyo mtu anayeapa kwa madhabahu, anaapa kwa hiyo madhabahu na vitu vyote vilivyoko juu yake. 21 Na mtu anapoapa kwa Hekalu, anaapa kwa hilo Hekalu na huyo aishie ndani yake. 22 Naye anayeapa kwa mbingu anaapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye aketiye juu ya kiti hicho.

23 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wana fiki! Kwa maana mnatoa fungu la kumi la mnanaa, na bizari na jira; lakini mmepuuza mambo makuu zaidi ya sheria: haki, huruma na imani. Haya mlipaswa kuyafanya bila kusahau yale mengine. 24 Ninyi viongozi vipofu, mnachuja nzi lakini mnameza ngamia!

25 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wana fiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje lakini ndani mmejaa ulafi na unyang’anyi. 26 Ninyi Mafarisayo vipofu! Kwanza safisheni kikombe na sahani kwa ndani, ndipo nje patakuwa safi.

27 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wana fiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa juu yanaonekana maridadi lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28 Hali kadhalika, nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

29 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wana fiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kupamba makaburi ya wenye haki 30 mkisema, ‘Kama tungaliishi wakati wa baba zetu tusingel ishiriki katika kuwaua manabii !’ 31 Kwa kusema hivyo mnakiri kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii. 32 Haya basi, kamilisheni hiyo kazi waliyoianza baba zenu! 33 Ninyi nyoka, ninyi kundi la nyoka! Mtaepukaje hukumu ya Jehena? 34 Kwa sababu hiyo nawapelekea manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwatundika msalabani, wengine mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na wengine mtawatesa toka mji mmoja hadi mji mwingine. 35 Na kwa hiyo damu ya wote wenye haki ambayo imemwagwa hapa duniani, tangu damu ya Abeli, ambaye alikuwa hana hatia, hadi damu ya Zakaria mwana wa Barakia ambaye mlimwua kati kati ya Patakatifu na madhabahu, itakuwa juu yenu. 36 Nawaambia kweli haya yote yatatokea wakati wa kizazi hiki.”

Yesu Awaonya Watu Wa Yerusalemu

37 “Ninyi watu wa Yerusalemu; mnawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwenu! Nilitamani sana kuwakusanya wana wenu kama vile kuku akusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, lakini hamkutaka! 38 Tazama nyumba yenu imeachwa tupu na ukiwa. 39 Kwa maana nawahakikishia kuwa, hamtaniona tena mpaka siku ile mtakaposema: ‘Amebarikiwa yeye anayekuja kwa jina la Bwana.

Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini

(Mk 12:38-40; Lk 11:37-52; 20:45-47)

23 Kisha Yesu akazungumza na watu pamoja na wafuasi wake, akasema, “Walimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kuwaambia Sheria ya Musa inasema nini. Hivyo mnapaswa kuwatii. Fanyeni kila wanachowaambia. Lakini maisha yao sio mfano mzuri wa kuufuata. Hawatendi wale wanayofundisha. Hutengeneza orodha ndefu ya kanuni na kujaribu kuwalazimisha watu kuzifuata. Lakini sheria hizi ni kama mizigo mizito ambayo watu hawawezi kuibeba, na viongozi hawa hawatazirahisisha kupunguza mzigo kwa watu.

Wao wanatenda mambo mema tu ili waonwe na watu wengine. Hufanya visanduku vidogo vya Maandiko[a] wanavyovaa kuwa vikubwa zaidi. Hufanya mashada ya urembo[b] kwenye mavazi yao ya nje kuwa marefu zaidi ili waonwe na watu. Watu hawa wanapenda kukaa sehemu za heshima kwenye sherehe na kwenye viti muhimu zaidi katika masinagogi. Wanapenda kuitwa ‘Mwalimu’ Na kusalimiwa kwa heshima na watu kwenye masoko.

Ninyi nyote ni ndugu, dada na kaka kwa sababu mnaye mwalimu mmoja tu. Hivyo msikubali kuitwa ‘Mwalimu’. Nanyi msimwite mtu yeyote duniani ‘Baba’, maana mnaye Baba mmoja tu, naye yuko mbinguni. 10 Msikubali kuitwa ‘Mwalimu’, kwa sababu mnaye Mwalimu mmoja tu, naye ni Masihi. 11 Kila atakayetumika kama mtumishi ndiyo mkuu zaidi kati yenu. 12 Wanaojifanya kuwa bora kuliko wengine watanyenyekezwa kwa lazima. Lakini watu wanaojinyenyekeza wenyewe watafanywa kuwa wakuu.

13 Ole wenu[c] walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnawafungia watu njia ya kuingia katika ufalme wa Mungu, kwa kuwa ninyi wenyewe hamwingii na mnawazuia wale wanaojaribu kuingia. 14 [d]

15 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki. Mnasafiri kuvuka bahari na nchi nyingine ili kumtafuta mtu mmoja atakayefuata njia zenu. Mnapompata mtu huyo, mnamfanya astahili maradufu kwenda Jehanamu kama ninyi mlivyo!

16 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona. Mnasema, ‘Mtu yeyote akiweka kiapo au nadhiri kwa jina la Hekalu, haimaanishi kitu. Lakini yeyote atakayeweka kiapo kwa kutumia dhahabu iliyo Hekaluni lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 17 Ninyi ni wasiyeona mlio wajinga! Hamwoni kuwa Hekalu ni kuu kuliko dhahabu iliyo ndani yake? Hekalu ndilo huifanya dhahabu kuwa takatifu!

18 Na mnasema, ‘Mtu yeyote akitumia madhabahu kuweka nadhiri au kiapo, haina maana yeyote. Lakini kila anayetumia sadaka iliyo kwenye madhabahu na kuapa au kuweka nadhiri, lazima atimize nadhiri au kiapo hicho.’ 19 Ninyi ni wasiyeona! Hamwoni kuwa madhabahu ni kuu kuliko sadaka yo yote iliyo juu yake? Madhabahu ndiyo inaifanya sadaka kuwa takatifu! 20 Kila anayeitumia madhabahu kuapa au kuweka nadhiri ni dhahiri anatumia madhabahu na kila kitu kilicho juu yake. 21 Na kila anayetumia Hekalu kuapa au kuweka nadhiri kwa hakika analitumia Hekalu na Mungu, anayeishi ndani humo. 22 Kila anayetumia mbingu kuapa au kuweka nadhiri anakitumia kiti cha enzi cha Mungu na yule aketiye juu yake.

23 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya chakula mnachopata,[e] hata mnanaa, binzari na jira.[f] Lakini hamtii mambo ya muhimu katika mafundisho ya sheria; kuishi kwa haki, kuwa wenye huruma, na kuwa waaminifu. Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya. Na mwendelee pia kufanya mambo hayo mengine. 24 Mnawaongoza watu lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona![g] Ninyi ni kama mtu anayemtoa nzi katika kinywa chake na kisha anammeza ngamia!

25 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnaosha vikombe na sahani zenu kwa nje. Lakini ndani yake vimejaa vitu mlivyopata kwa kuwadang'anya wengine na kujifurahisha ninyi wenyewe. 26 Mafarisayo, ninyi ni wasiyeona! Safisheni kwanza vikombe kwa ndani ili viwe safi. Ndipo vikombe hivyo vitakuwa safi hata kwa nje.

27 Ole wenu walimu wa sheria na ninyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Ninyi ni kama makaburi yaliyopakwa rangi nyeupe, lakini ndani yake yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28 Ndivyo ilivyo hata kwenu. Watu wanawatazama na kudhani kuwa ninyi ni wenye haki, lakini mmejaa unafiki na uovu ndani yenu.

29 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii, na kuyaheshimu makaburi ya wenye haki waliouawa. 30 Na mnasema, ‘Ikiwa tungeishi nyakati za mababu zetu, tusingewasaidia kuwaua manabii hawa.’ 31 Hivyo mnathibitisha kuwa ninyi ni uzao wa wale waliowaua manabii. 32 Na mtaimalizia dhambi waliyoianza mababu zenu!

33 Enyi nyoka! Ninyi mlio wa uzao wa nyoka wenye sumu kali! Hamtaikwepa adhabu. Mtahukumiwa na kutupwa Jehanamu! 34 Hivyo ninawaambia: Ninawatuma manabii na walimu wenye hekima na wanaojua Maandiko. Lakini mtawaua, mtawatundika baadhi yao kwenye misalaba na kuwapiga wengine katika masinagogi yenu. Mtawafukuza kutoka katika mji mmoja hadi mwingine.

35 Hivyo mtakuwa na hatia kutokana vifo vyote vya watu wema wote waliouawa duniani. Mtakuwa na hatia kwa kumwua mtu wa haki Habili, na mtakuwa na hatia kwa kuuawa kwa Zakaria[h] mwana wa Barakia mliyemwua kati ya Hekalu na madhabahu. Mtakuwa na hatia ya kuwaua watu wote wema walioishi kati ya wakati wa Habili mpaka wakati wa Zakaria. 36 Niaminini ninapowaambia kuwa mambo haya yote yatawapata ninyi watu mnaoishi sasa.

Yesu Awaonya Watu wa Yerusalemu

(Lk 13:34-35)

37 Ee Yerusalemu, Yerusalemu! Unayewaua manabii. Unawapiga kwa mawe wale ambao Mungu amewatuma kwako. Mara nyingi nimetaka kuwasaidia watu wako. Nimetaka kuwakusanya watu wako kama kuku anavyowakusanya vifaranga wake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu kufanya hivyo. 38 Sasa Hekalu lako litaachwa ukiwa kabisa. 39 Ninakwambia, hautaniona tena mpaka wakati utakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(A)

Footnotes

  1. 23:5 visanduku vidogo vya Maandiko Visanduku vidogo vya ngozi vyenye Maandiko manne muhimu. Baadhi ya Wayahudi walivifunga visanduku hivi kwenye vipaji vya nyuso zao na mkono wa kushoto kuonesha kumpenda au uaminifu wao kwa Mungu na Neno lake. Mafarisayo wengi walitengeneza visanduku hivi vikubwa kuliko vya wengine kuonesha kuwa wao ni watu wa dini kuliko watu wengine.
  2. 23:5 mashada ya urembo Urembo uliotengenezwa kwa nyuzi za sufu au manyoya ya kondoo zinazotambaa mpaka chini kutoka pembe nne za vazi la kusalia au vazi la maombi lililovaliwa na Wayahudi. Urembo huu ulipaswa kuwa ukumbusho wa amri za Mungu (tazama Hes 15:38-41).
  3. 23:13 Ole wenu Ama Itakuwa vibaya kwenu enyi walimu wa sheria na Mafarisayo.
  4. 23:14 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 14: “Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo. Ninyi ni wanafiki. Mnawadanganya wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha mnafanya maombi marefu ili watu wawaone. Mtapata adhabu mbaya zaidi.” Tazama Mk 12:40; Lk 20:47.
  5. 23:23 Mnampa Mungu … mnachopata Sheria ya Musa iliwataka Waisraeli kumtolea Mungu sehemu ya kumi ya mazao yao (tazama Law 27:30-32; Kum 26:12).
  6. 23:23 mnanaa, binzari na jira Haya ni mazao yaliyotolewa malipo ya fungu la kumi. Lakini sheria ya Musa halikujumuisha mazao madogo kama haya yaliyotajwa hapa. Bali Mafarisayo walikuwa wanatoa zaidi ili kuwa na uhakika kuwa hawavunji Sheria.
  7. 23:24 lakini ninyi wenyewe ni wasiyeona Hii ina maana kuwa “Mnajishughulisha kwa mambo madogo sana lakini mnatenda dhambi kubwa.”
  8. 23:35 Habili, Zakaria Katika Agano la Kale la Kiebrania, hawa ni watu wa kwanza na wa mwisho kuuawa. Tazama Mwa 4:8-11 na 2 Nya 24:20-25.