Add parallel Print Page Options

Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa

(Mt 9:18-26; Mk 5:21-43)

40 Yesu aliporudi Galilaya, watu walimkaribisha. Kila mtu alikuwa anamsubiri. 41-42 Mtu mmoja jina lake Yairo, aliyekuwa mkuu wa sinagogi alimwendea. Alikuwa na binti mmoja tu mwenye umri wa miaka kumi na mbili na alikuwa mgonjwa sana katika hali ya kufa. Hivyo Yairo alisujudu miguuni pa Yesu na akamsihi aende nyumbani kwake.

Yesu alipokuwa akienda nyumbani kwa Yairo, watu walimzonga kila upande. 43 Mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili alikuwepo katika umati huo. Alikuwa ametumia mali zake zote kwa madaktari,[a] lakini hakuna daktari aliyeweza kumponya. 44 Alikwenda nyuma ya Yesu na kugusa pembe ya vazi lake. Wakati huo huo damu ikaacha kumtoka. 45 Ndipo Yesu akasema, “Nani amenigusa?”

Kila mtu alikataa kuwa hajamgusa, Petro akasema, “Mkuu, watu wamekuzunguka na wanakuzongazonga kila upande.”

46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu amenigusa. Nimesikia nguvu ikinitoka.” 47 Yule mwanamke alipoona ya kwamba hataweza kujificha akajitokeza akitetemeka. Akasujudu mbele ya Yesu. Huku kila mmoja akisikia, akaeleza sababu iliyomfanya amguse, na kwamba alipona wakati ule ule alipomgusa. 48 Yesu alimwambia, “Binti yangu umeponywa kwa sababu uliamini. Nenda kwa amani.”

49 Yesu alipokuwa bado anaongea, mtu mmoja kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi alikuja na akasema, “Binti yako amekwisha kufa! Hakuna haja ya kuendelea kumsumbua Mwalimu.”

50 Yesu aliposikia maneno hayo, alimwambia Yairo, “Usiogope! Amini tu na binti yako ataponywa.”

51 Yesu akaenda nyumbani, alipofika akaruhusu Petro, Yohana, Yakobo pamoja na baba na mama wa yule mtoto tu kuingia ndani pamoja naye. 52 Kila mtu alikuwa akilia na kusikia huzuni kwa sababu msichana alikuwa amekufa. Lakini Yesu akasema, “Msilie. Hajafa. Amelala usingizi tu.”

53 Watu wakamcheka, kwa sababu walijua kuwa amekwisha kufa. 54 Lakini Yesu akamshika mkono na kumwambia, “Mtoto inuka!” 55 Roho yake ikamrudia, akasimama hapo hapo. Yesu akasema, “Mpeni chakula.” 56 Wazazi wa yule binti wakashangaa. Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote lililotokea.

Read full chapter

Footnotes

  1. 8:43 Alikuwa ametumia … madaktari Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya.