Add parallel Print Page Options

Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi

(Mt 4:18-22; Mk 1:16-20)

Yesu aliposimama ukingoni mwa Ziwa Galilaya[a] kundi la watu lilimsogelea ili wasikie mafundisho kuhusu Mungu. Yesu aliona mashua mbili zikiwa kando ya ziwa. Wavuvi walikuwa wametoka katika mashua zao na walikuwa wanaosha nyavu zao. Yesu aliingia kwenye mashua ya Simoni. Akamwomba Simoni aisogeze mbali kidogo na ufukwe wa ziwa. Kisha akaketi ndani ya mashua na akawafundisha watu waliokuwa ufukweni mwa ziwa.

Yesu alipomaliza kufundisha, alimwambia Simoni, “Ipeleke mashua mpaka kwenye kilindi cha maji kisha mshushe nyavu zenu majini na mtapata samaki.”

Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi usiku kucha kuvua samaki na hatukupata chochote. Lakini kwa kuwa unasema nishushe nyavu majini, nitafanya hivyo.” Walipofanya hivi, nyavu zao zilijaa samaki wengi mpaka zikaanza kuchanika. Waliwaita rafiki zao waliokuwa katika mashua nyingine ili waje wawasaidie. Rafiki zao walikuja kuwasaidia, na mashua zote mbili zilijaa samaki kiasi cha kutaka kuzama.

8-9 Wavuvi wote walistaajabu kwa sababu ya wingi wa samaki waliovua. Simoni Petro alipoona hili, akapiga magoti mbele ya Yesu na akasema, “Nenda mbali nami Bwana, mimi ni mwenye dhambi!” 10 Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo, walishangaa pia. (Yakobo na Yohana walikuwa wanavua pamoja na Simoni.)

Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope. Kuanzia sasa kazi yako haitakuwa kuvua samaki bali kukusanya watu!”

11 Wakaziendesha mashua zao mpaka pwani, kisha wakaacha kila kitu na kumfuata Yesu.

Read full chapter

Footnotes

  1. 5:1 Galilaya Kwa maana ya kawaida, “Genesareti”.