Add parallel Print Page Options

Simulizi Kuhusu Watumishi Watatu

(Mt 25:14-30)

11 Kundi la watu walipokuwa bado wanamsikiliza Yesu akizungumza mambo haya. Akaongeza kwa kuwasimulia simulizi hii. Na sasa alikuwa karibu na mji wa Yerusalemu na watu walidhani kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa unakwenda kutokea haraka. 12 Akasema, “Mtu mmoja maarufu alikuwa anajiandaa kwenda katika nchi ya mbali kutawazwa kuwa mfalme. Kisha arudi nyumbani na kuwatawala watu wake. 13 Hivyo aliwaita watumishi wake kumi kwa pamoja. Akampa kila mtumishi fungu la pesa.[a] Akamwambia kila mtumishi, ‘Zifanyie biashara pesa hizi mpaka nitakaporudi.’ 14 Lakini watu katika ule ufalme walikuwa wanamchukia mtu huyu na hivyo walituma kundi la watu kwenda katika nchi nyingine. Walipofika huko wakasema, ‘Hatutaki mtu huyu awe mfalme wetu.’

15 Lakini mtu yule akatawazwa kuwa mfalme. Aliporudi nyumbani, akaagiza akasema, ‘Waiteni wale watumishi wenye pesa zangu. Ninataka kujua wamezalisha kiasi gani kutokana na pesa hizo.’ 16 Mtumishi wa kwanza alikuja na akasema, ‘Mkuu, nilizalisha mafungu kumi ya pesa kutokana na fungu moja ulilonipa.’ 17 Mfalme akamwambia, ‘Vizuri sana! Wewe ni mtumishi mwema. Nilikuamini kwa vitu vidogo, lakini sasa utakuwa mtawala wa miji yangu kumi.’

18 Mtumishi wa pili akasema, ‘Mkuu, kwa fungu moja la pesa zako, nilizalisha mafungu matano.’ 19 Mfalme akamwambia mtumishi huyu, ‘Utatawala miji yangu mitano.’

20 Kisha mtumishi mwingine akaingia na akasema, ‘Mkuu, fungu lako la pesa hili hapa. Nilizifunga katika kipande cha nguo na kulificha. 21 Niliogopa kwa sababu wewe ni mgumu. Unachukua hata pesa ambazo hukuzizalisha na kukusanya chakula ambacho hukupanda.’

22 Kisha mfalme akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya! Nitatumia maneno yako mwenyewe kukuhukumu. Unasema kuwa mimi ni mtu mgumu, ninachukua hata pesa ambazo sikuzizalisha na nakusanya chakula ambacho sikupanda? 23 Ikiwa hiyo ni kweli, ulipaswa kuweka pesa zangu kwa watoao riba. Ili nitakaporudi pesa hiyo iwe imezalisha faida.’ 24 Kisha mfalme akawaambia watu waliokuwa pale, ‘Mnyang'anyeni mtumishi huyu fungu la pesa na mpeni mtumishi aliyezalisha mafungu kumi ya pesa.’

25 Lakini watu wakamwambia mfalme, ‘Mkuu, yule mtumishi ana mafungu kumi tayari.’

26 Mfalme akasema, ‘Waliozalisha faida watapata zaidi. Lakini ambao hawakuzalisha faida watanyang'anywa kila kitu. 27 Sasa, adui zangu wako wapi? Wako wapi watu ambao hawakutaka niwe mfalme? Waleteni adui zangu hapa na waueni huku nikiangalia wanavyokufa.’”

Read full chapter

Footnotes

  1. 19:13 fungu la pesa Fungu moja la pesa kwa Kiyunani liliitwa mina, ambayo ni sarafu 100 za fedha, uliotosha kumlipa mtu mshahara kwa miezi mitatu. Pia katika mstari wa 16,18,20,24 na 25.