Makao Ya Mbinguni

Kwa maana twajua kwamba kama hema hii tunamoishi tukiwa ulimwenguni itaharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba ya milele mbinguni, ambayo haikujengwa kwa mikono ya wanadamu. Maana sasa twaugua, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena tukiwa uchi. Tukiwa bado tunaishi katika hema hii tunaugua na kulemewa, kwa maana hatutaki kukaa bila nguo bali tunatamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili ile hali ya kufa imezwe na uhai. Mungu ndiye aliyetuandaa kwa shabaha hii, naye ametupa Roho wake kama mdha mana, kutuhakikishia mambo yajayo baadaye. Kwa hiyo wakati wote tuna ujasiri mkuu. Tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na nyumbani kwa Bwana. Tunaishi kwa imani na si kwa kuona. Nasema tuna ujasiri na ingekuwa afadhali kuuacha mwili huu tukaishi nyumbani na Bwana. Kwa hiyo, kama tuko nyumbani katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana. 10 Kwa kuwa sisi sote inatubidi kusimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo. Na kila mmoja atapokea mema au mabaya, kulingana na matendo yake alipokuwa katika mwili.

Huduma Ya Upatanisho

11 Kwa hiyo tukijua umuhimu wa kumcha Bwana tunajaribu kuwa vuta watu. Mungu anatufahamu fika. Tunaamini kwamba dhamiri zenu pia zinatufahamu tulivyo. 12 Hatujaribu kujipendekeza kwenu tena, lakini tunataka kuwapeni nafasi mjisifu juu yetu ili muweze kuwajibu hao wanaojisifia mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni. 13 Kama tumeehuka, ni kwa ajili ya Mungu; lakini kama tuna akili timamu ni kwa faida yenu. 14 Kwa kuwa upendo wa Kristo unatusukuma, tunaamini ya kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote kwa hiyo wote walikufa. 15 Naye alikufa kwa ajili ya watu wote ili wote wanaoishi, wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuka tena kwa ajili yao.

16 Tangu sasa hatumtazami mtu ye yote namna ya kibinadamu, ingawaje hapo mwanzo tulimtazama Kristo kwa namna ya kibinadamu. Hatumtazami hivyo tena. 17 Kwa hiyo mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, mapya yamekuja. 18 Haya yote yanatoka kwa Mungu, ambaye kwa njia ya Yesu Kristo ametupatanisha na mwenyewe, na akatupa huduma ya upatanisho. 19 Ndani ya Kristo Mungu aliupatanisha ulimwengu na yeye mwe nyewe, asiwahesabie watu dhambi zao. Naye ametukabidhi ujumbe huu wa upatanisho.

20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, Mungu anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Na sisi tunawasihi ninyi kwa niaba ya Kristo: mpatanishwe na Mungu. 21 Mungu alimfanya yeye ambaye hakujua dhambi, awe dhambi kwa ajili yetu ili ndani yake tupate kuwa haki ya Mungu.

Tunafahamu kuwa miili yetu, ambayo ni hema tunaloishi ndani yake hapa duniani itaharibiwa. Hilo litakapotokea, Mungu atakuwa na nyumba tayari kwa ajili yetu kuishi ndani yake. Haitakuwa nyumba kama ambayo watu hujenga hapa duniani. Itakuwa nyumba ya mbinguni itakayodumu milele. Lakini wakati bado tunaishi katika miili hii, tunaugua kwa sababu tuna shauku kubwa mbele za Mungu ya kutupa mwili wetu mpya wa mbinguni ili tuweze kujivika. Tutauvaa mwili wa mbinguni kama vazi jipya na hatutakuwa uchi. Tunapoishi katika “hema” hili la kidunia, tunaugua na kuelemewa na mizigo. Lakini, hiyo si kwa sababu tunataka kuivua miili hii ya zamani. Hapana, ni kwa sababu tunataka kuivaa miili yetu mipya. Kisha mwili huu unao kufa utafunikwa na uzima. Hii ndiyo sababu Mungu mwenyewe ndiye aliyetuandaa kwa kusudi hili hasa. Na ametupata Roho kama malipo ya awali kutuhakikishia maisha yajayo.

Hivyo tuna ujasiri daima. Tunafahamu kuwa tunapoendelea kuishi katika mwili huu, tunakuwa mbali na makao yetu pamoja na Bwana. Tunaishi kwa msingi wa yale tunayoamini kuwa yatatokea na siyo kwa msingi wa yale tunayoyaona. Hivyo ninasema tuna ujasiri. Na tungependa kuondoka na kutokuwa katika mwili huu na kuwa nyumbani pamoja na Bwana. Lengo letu pekee ni kumpendeza Bwana, kwamba tupo nyumbani au mbali. 10 Tutasimama sote mbele za Kristo ili tuhukumiwe. Kila mtu atalipwa anachostahili. Kila mtu atalipwa kutokana na matendo yake, mazuri au mabaya, alipoishi katika mwili huu wa kidunia.

Kuwasaidia Watu Ili Wawe Rafiki wa Mungu

11 Tunafahamu maana ya kuwa na hofu na Bwana, hivyo tunajitahidi kuwashawishi watu waipokee. Mungu anafahamu tulivyo, na ni matarajio yangu kuwa nanyi mioyoni mwenu mnatufahamu sisi pia. 12 Hatujaribu tena kujithibitisha kwenu sasa. Lakini tunawapa sababu za ninyi kujivuna kwa ajili yetu. Kisha mtaweza kuwa na majibu kwa ajili wanaojivuna kwa ajili ya yale yanayoonekana. Hawajali kuhusu kilicho katika moyo wa mtu. 13 Ikiwa tuna wazimu, ni kwa ajili ya Mungu na ikiwa tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu. 14 Upendo wa Kristo unatutawala, kwa sababu tunafahamu kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote. Hivyo wote wamekufa. 15 Alikufa kwa ajili ya wote ili wanaoishi wasiendelee kuishi kwa ajili yao wenyewe. Alikufa kwa ajili yao na alifufuka toka kwa wafu ili waishi kwa ajili yake.

16 Kuanzia sasa hatumfikirii mtu yeyote kama ulimwengu unavyowafikiria watu. Ni kweli kuwa zamani kale tulimfikiria Kristo kwa mtazamo wa kidunia. Lakini hatufikirii hivyo sasa. 17 Mtu anapokuwa ndani ya Kristo, anakuwa kiumbe[a] kipya kabisa. Mambo ya zamani yanakoma; na ghafla kila kitu kinakuwa kipya! 18 Yote haya yatoka kwa Mungu. Kupitia Kristo, Mungu alifanya amani katika yake na sisi. Na Mungu alitupa kazi ya kuleta amani kati ya watu na Mungu. 19 Tunachosema ni kuwa kupitia Kristo, Mungu alikuwa anaweka amani kati yake na ulimwengu. Alikuwa anatoa ujumbe wa msamaha kwa kila mtu kwa matendo mabaya waliyotenda kinyume naye. Na alitupa ujumbe huu wa amani ili kuwaeleza watu. 20 Hivyo tumetumwa kwa ajili ya Kristo. Ni kama Mungu anawaita watu kupitia sisi. Tunazungumza kwa niaba ya Kristo tunapowasihi ninyi kuwa na amani na Mungu. 21 Kristo hakuwa na dhambi,[b] ila Mungu alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu ili ndani ya Kristo tuweze kufanyika kielelezo cha wema wa uaminifu wa Mungu.

Footnotes

  1. 5:17 Kiumbe kipya Au “Mtu anapokuwa ndani ya Kristo anakuwa katika ulmwengu mpya.”
  2. 5:21 hakuwa na dhambi Au “hakuwa sadaka ya dhambi”.