Kutoka kwa Paulo mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu. Kwa Kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watu wote wa Mungu walioko Akaya yote.

Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Faraja Katika Mateso

Ashukuriwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja zote. Yeye anatufariji katika mateso yetu yote ili tuweze kuwafariji wale walio katika mateso yo yote, tukitumia faraja ambayo sisi tumepokea kutoka kwa Mungu. Kama vile tunavyoshiriki mateso ya Kristo yaliyo mengi, ndivyo na far aja yetu inavyomiminika kwa wengine. Kama tunateseka ni kwa faraja yenu na wokovu wenu; kama tukifarijiwa, ni kwa faraja yenu, ambayo mnapata wakati mkivumilia kwa subira mateso hayo hayo tunayopata sisi. Matumaini yetu kwenu ni imara; kwa maana tunajua ya kuwa kama mnavyoshiriki katika mateso yetu, mtashiriki pia katika faraja yetu.

Hatupendi mkose kujua, ndugu wapendwa, kuhusu mateso tuliy oyapata huko Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo ambayo ilikuwa zaidi ya uwezo wetu kuvumilia, kiasi kwamba tulikata tamaa kwamba tungeishi. Kwa hakika tulijisikia kana kwamba tumehukumiwa kifo. Lakini hii ilitokea ili tusijitegemee wenyewe bali tumtege mee Mungu ambaye anawafufua wafu. 10 Alituokoa katika hatari hiyo ya kifo, na atatuokoa. Tumeweka tumaini letu juu yake kwamba ataendelea kutuokoa. 11 Ninyi pia mtusaidie kwa maombi ili wengi wamshukuru Mungu kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka tulizopokea kama majibu ya maombi ya wengi.

Paulo Abadili Mipango Yake

12 Hii ndio sababu tunajivuna. Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeishi katika ulimwengu, na hasa katika uhusiano wetu na ninyi, kwa utakatifu na ukweli utokao kwa Mungu. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya mwanadamu bali kwa neema ya Mungu. 13 Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma na kuyaelewa. Natumaini mtaelewa kikamilifu, 14 yale ambayo sasa mnayaelewa kwa sehemu, ili siku ile ya Bwana Yesu muweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu.

15 Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilipanga kuwatembelea kwanza ili mpate baraka mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia, na kurudi kwenu tena nikitoka Makedonia ili mnisaidie katika safari yangu ya kwenda Uyahudi. 17 Je, nilikuwa kigeugeu nilipotaka kufanya hivi? Au mimi ninafanya mipango yangu kama watu wa dunia, nikiwa tayari kusema, “Ndiyo” na wakati huo huo kusema, “Hapana”?

18 Lakini kama Mungu alivyo mwaminifu, ahadi yangu haikuwa “Ndiyo” na “Hapana” 19 Kwa kuwa Mwana wa Mungu Yesu Kristo, ambaye tulimhubiri kwenu tukiwa na Silvano, Timotheo, na mimi mwenyewe, hakuwa ‘ndio’ na ‘hapana.’ Katika yeye wakati wote ni ndio. 20 Kwa maana ahadi zote za Mungu ni ‘ndio’ katika Kristo. Ndio sababu tunatamka ‘Amina’ kwa ajili yake, kwa utukufu wa Mungu. 21 Ni Mungu mwenyewe ambaye anatuwezesha sisi na ninyi kusimama imara katika Kristo. Ametuweka wakfu; 22 ametutia mhuri wake juu yetu, akatupa Roho wake mioyoni mwetu kama uthibitisho.

23 Mungu ni shahidi wangu kwamba niliacha kurudi Korintho kwa kuwahurumia. 24 Hatutaki kuwaamrisha kuhusu imani yenu bali tunafanya kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu; kwa maana mnasimama imara kwa imani.

Salamu kutoka kwa Paulo, Mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alitaka. Na Timotheo ndugu yetu katika Kristo.

Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho na kwa watakatifu wote wa Mungu walio jimbo lote la Akaya.

Neema na Amani iwe kwenu kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Paulo Anamshukuru Mungu

Sifa na zimwendee Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni baba aliyejaa rehema, Mungu aliye mwingi wa faraja. Hutufariji kila wakati tunapokuwa katika hali ya matatizo ili wengine wawapo katika matatizo, tuweze kuwafariji kwa namna ile ile ambayo Mungu ametufariji sisi. Twashiriki katika mateso mengi ya Kristo. Na kwa namna hiyo hiyo, faraja nyingi hutujia kwa njia ya Kristo. Ikiwa tuko katika mateso, tuko kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu. Na ikiwa tunafarijika, ni kwa sababu tuweze kuwafariji ninyi. Hili huwasaidia katika kuyakubali mateso yale yale tunayopata kwa uvumilivu. Tumaini letu kwenu liko imara. Tunafahamu kuwa mnashiriki katika mateso yetu. Hivyo tunafahamu pia kuwa mnashiriki katika faraja yetu pia.

Ndugu zangu, tunapenda mfahamu juu ya mateso tuliyoyapata hapa Asia. Tulikuwa na mzigo sana huko, ulikuwa mzito kuliko hata nguvu zetu. Hata tulipoteza tumaini la kuishi. Ukweli ni kuwa, ilionekana kana kwamba Mungu alikuwa anatuambia kuwa tunakwenda kufa. Lakini haya yalitokea ili tusizitumainie nguvu zetu bali tumtumainie Mungu, ambaye huwainua watu toka mautini. 10 Yeye alituokoa toka katika hatari hizi kubwa za mauti, na ataendelea kutuokoa. Twajisikia kuwa na hakika kuwa ataendelea kutuokoa. 11 Nanyi mnaweza kutusaidia kwa njia ya maombi. Ndipo watu wengi wataweza kumshukuru Mungu kwa ajili yetu; kwamba Mungu alitubariki kutokana na maombi yao mengi.

Mabadiliko katika Mipango ya Paulo

12 Hili ndilo tunalojivunia, na naweza kusema kwa dhamiri safi kwamba ni kweli: Katika kila kitu tulichofanya duniani, Mungu ametuwezesha kukifanya kwa moyo safi. Na hili ni kweli zaidi katika yale tuliyowatendea ninyi. Tulifanya hivyo kwa neema ya Mungu, si kwa hekima ambayo ulimwengu unayo. 13 Tunawaandikia mambo mnayoweza kusoma na kuyaelewa. Na nina matumaini kuwa mtayaelewa inavyopasa 14 kama ambavyo tayari mmekwisha kuyafahamu mambo mengi kuhusu sisi. Natumaini mtaelewa kuwa mnaweza kuona fahari juu yetu, kama nasi tutakavyoona fahari juu yenu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja.

15 Nilikuwa na uhakika sana juu ya haya yote. Ndiyo maana niliweka mpango wa kuwatembelea kwanza. Kisha mngebarakikwa mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nilipokuwa nikienda Makedonia na nilipokuwa ninarudi. Na nilipanga kuwaomba mniletee kutoka huko hadi Yudea chochote ambacho nilihitaji kwa ajili ya safari yangu. 17 Je! Mnadhani nilipanga mipango hii bila kufikiri? Au mnadhani ninafanya mipango kama vile dunia inavyofanya, lugha yetu kwenu si ndiyo na hapana kwa wakati mmoja.

18 Kama ambavyo kwa hakika mnaweza kumwamini Mungu, basi mnaweza kuamini kuwa lile tunalowaambia kamwe haliwezi kuwa ndiyo na hapana kwa pamoja. 19 Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, Yeye ambaye Sila, Timotheo, na mimi tuliwaeleza habari zake, hakutokea kuwa ni ndiyo na hapana kwa ahadi za Mungu. Kinyume chake ndiyo ya Mungu imethibitika daima katika Kristo kuwa ni ndiyo. 20 Ndiyo kwa ahadi zote za Mungu katika Kristo. Na hii ndiyo maana twasema “Amina” Katika Kristo kwa utukufu wa Mungu. 21 Na Mungu ndiye anayewafanya ninyi na sisi kuwa imara katika Kristo. Mungu pia ndiye aliyetuchagua kwa ajili ya kazi yake.[b] 22 Aliweka alama yake juu yetu ili kuonesha kuwa tu mali yake. Ndiyo, amemweka roho wake ndani ya mioyo yetu kama malipo ya awali yanayotuhakikishia mambo yote atakayotupa.

23 Ninawaambia hili, na ninamwomba Mungu awe shahidi wangu kuwa ni la kweli: Sababu iliyonifanya nisirudi tena Korintho ni kuwa nilitaka niepuke kuwapa karipio lenye nguvu. 24 Sina maana ya kuwa tunataka kuitawala imani yenu. Ninyi mpo imara katika imani. Lakini tunatenda kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu wenyewe.

Footnotes

  1. 1:1 Kristo Yesu Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32: Lk 23:2. Tazama pia Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  2. 1:21 aliyetuchagua … kazi yake Kwa maana ya kawaida, “alitupaka mafuta.” Kwa Kiyunani neno hili linahusiana na “Kristo” ambalo linatafsiriwa kama “mpakwa mafuta.” Tazama Kristo katika Orodha ya Maneno.