Kushtakiana Kati Ya Ndugu

Kama mmoja wenu ana mashtaka kumhusu ndugu, anathubutuje kupeleka mashtaka yake mbele ya mahakimu wasio mcha Mungu, badala ya kuyapeleka mbele ya watu wa Mungu? Hamjui kwamba watu wa Mungu watahukumu ulimwengu? Na kama ninyi mtahukumu ulimwengu, hamwezi kuhukumu mambo madogo madogo? Hamjui kwamba tutawahu kumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? Kwa hiyo kwa nini kama kuna kutokuelewana kati yenu kuhusu mambo kama haya, mnachagua kama mahakimu watu ambao hata hawaheshimiwi na kanisa? Nasema hivi ili muone aibu. Je, inawezekana kuwa hakuna mtu kati yenu mwenye hekima ya kutosha kuamua mashtaka kati ya ndugu mmoja na mwenzake? Badala yake ndugu mmoja anampeleka ndugu mwingine mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!

Kwamba mnashtakiana kati yenu ni dalili kuwa mmeanguka. Badala ya kushtakiana, kwa nini msikubali kutendewa ubaya? Kwa nini msikubali kudanganywa? Lakini ninyi wenyewe mnakoseana na kudhulumiana, na mnafanya hivyo hata kwa ndugu zenu!

Je, hamjui kwamba wasio na haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike, waasherati hawataurithi Ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wapotoshaji; 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyang’anyi. 11 Na baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

Dhambi Za Zinaa

12 “Kila kitu ni halali kwangu,”lakini si kila kitu kina faida. “Kila kitu ni halali kwangu,”lakini sitatawaliwa na cho chote. 13 “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula,” lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mwanadamu haukuumbwa kwa ajili ya zinaa bali kwa ajili ya Bwana, na Bwana kwa ajili ya mwili.

14 Mungu alimfufua Bwana na atatufufua na sisi pia kwa uwezo wake. 15 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni sehemu ya Kristo? Je, naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuiunganisha na mwili wa kahaba? Hata kidogo! 16 Hamjui kwamba mtu aushirikishaye mwili wake na kahaba ana kuwa mmoja naye kimwili? Maandiko yanasema, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 17 Lakini mtu anayejiunga na Bwana ana kuwa mmoja naye kiroho.

18 Kimbieni dhambi ya zinaa. Dhambi nyingine zote anazotenda mwanadamu hufanyika nje ya mwili wake, lakini anayezini, ana tenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. 19 Hamjui kwamba miili yenu ni Hekalu la Roho Mtakatifu anayekaa ndani yenu, ambaye mme pewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe; 20 mmenunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.

Kutatua Migogoro Miongoni Mwa Waamini

Kwa nini mnakwenda kwenye mahakama za kisheria mmoja wenu anapokuwa na shauri dhidi ya mwingine aliye miongoni mwenu? Mnajua ya kwamba mahakimu wa aina hiyo hawawezi kutegemewa kuamua kwa haki iliyo ya kweli. Sasa kwa nini mnawaruhusu wawaamulie aliye na haki? Kwa nini msiwaruhusu watakatifu wa Mungu waamue ni nani aliye na haki? Hamjui kuwa watakatifu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Hivyo, ikiwa mtauhukumu ulimwengu, hakika mnaweza kutatua mashauri kama hayo miongoni mwenu. Hakika mnajua kuwa tutawahukumu malaika. Kwa kuwa hiyo ni kweli basi hakika tunaweza kuhukumu masuala ya kawaida ya maisha. Sasa, ikiwa mna masuala kama haya ya kawaida ya maisha yanayotakiwa kuamuliwa, kwa nini mnayapeleka kwa wasio waamini? Hao ambao hawana umuhimu wo wote kwenu? Ninasema hivi ili kuwatahayarisha. Nina uhakika yupo mwenye hekima miongoni mwa waamini katika kanisa lenu anayeweza kutatua mgogoro kati ya waamini wawili. Lakini sasa mwamini mmoja anamshtaki mwamini mwenzake na mnaruhusu watu wasio waamini wawaamulie!

Ule ukweli kuwa mnayo mashitaka baina yenu ninyi kwa ninyi tayari ni uthibitisho wa kushindwa kwenu kabisa. Ingekuwa bora kwenu kustahimili yasiyo haki ama kulaghaiwa. Lakini ninyi ndiyo mnaotenda mabaya kwa kudanganya. Na mnawafanyia hivi ndugu zenu katika Kristo!

Msijidanganye. Hamjui ya kuwa wanaowatendea mabaya hawana nafasi katika ufalme wa Mungu. Ninasema kuhusu wazinzi, wanaoamini miungu wa uongo, wasio waaminifu katika ndoa, nao wanaolawitiana.[a] 10 Pia wezi, walafi, walevi, watukanaji, au waongo wanaowadanganya wengine ili wawaibie hawatakuwa na sehemu katika ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa hivyo huko nyuma. Lakini mlisafishwa mkawa safi, mkafanywa kuwa watakatifu na mkahesabiwa haki na Mungu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.

Miili Yenu Itumike kwa Ajili ya Utukufu wa Mungu

12 Mtu mmoja anaweza kusema, “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote.” Nami ninawaambia ya kuwa si vitu vyote vilivyo na manufaa. Hata kama ni kweli kuwa “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote,” Sitaruhusu kitu chochote kinitawale kama vile ni mtumwa. 13 Mmoja wenu anasema, “Chakula ni kwa ajili ya tumbo na tumbo ni kwa ajili ya chakula, na Mungu ataviteketeza vyote.” Hiyo ni dhahiri, lakini mwili si kwa ajili ya zinaa, bali kwa ajili ya Bwana, na Bwana ni kwa ajili ya mwili. 14 Na Mungu ataifufua pia miili yetu kutoka kwa wafu kwa nguvu yake, kama alivyomfufua Bwana Yesu. 15 Hakika mnajua kuwa miili yenu ni sehemu ya Kristo mwenyewe. Hivyo sitakiwi kamwe kuchukua sehemu ya Kristo na kuiunganisha na kahaba! 16 Maandiko yanasema, “Watu wawili watakuwa mmoja.”(A) Hivyo mnapaswa kujua kuwa kila aliyeungana na kahaba, amekuwa mwili mmoja na kahaba. 17 Lakini aliyeungana na Bwana, yu mmoja naye katika roho.

18 Hivyo ikimbieni dhambi ya uzinzi. Mnasema kuwa, “Kila dhambi ni kitu kilichomo katika akili tu haihusiki na mwili.” Lakini ninawaambia, anayetenda dhambi ya uzinzi anautendea dhambi mwili wake mwenyewe. 19 Nina uhakika mnajua kuwa mwili wenu ni hekalu[b] kwa ajili ya Roho Mtakatifu mliyepewa na Mungu na Roho Mtakatifu anaishi ndani yenu. Hamjimiliki ninyi wenyewe. 20 Mungu alilipa gharama kubwa ili awamiliki. Hivyo mtukuzeni Yeye kwa kutumia miili yenu.

Footnotes

  1. 6:9 wanaolawitiana Neno la Kiyunani linajumuisha wale wanaolawitiwa na wale wanaolawiti. Ina maana ya “[wanaume] waliolegea”, wenye haiba ya kike wanaokosa uthabiti walio nao wanaume. Hii ni pamoja na wanaume ambao kwa kawaida wanashiriki matumizi ya wanawake.
  2. 6:19 hekalu Nyumba ya Mungu, mahali ambapo watu wa Mungu humwabudu. Hapa, inamaanisha kuwa waamini ndiyo hekalu la kiroho ambamo Mungu anaishi.