Mgawanyiko Katika Kanisa

Lakini ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwili, na kama watoto wachanga katika Kristo. Niliwalisha maziwa, sio chakula kigumu; kwa kuwa mli kuwa hamjawa tayari kukipokea. Kwa maana ninyi bado mnatawaliwa na mambo ya mwili. Je, wakati kuna wivu na kugombana kati yenu, ninyi si watu wa mwili wenye tabia kama za watu wa kawaida? Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo” hamfanyi kama watu wa kawaida?

Hata hivyo, Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Sisi ni watum ishi tu ambao kama Bwana alivyotupangia kila mmoja kazi yake, mliamini kwa msaada wetu. Mimi nilipanda mbegu, na Apolo akaimwagilia maji, lakini ni Mungu aliyefanya mbegu iote. Kwa hiyo anayepanda mbegu na anayemwagilia maji si kitu, bali Mungu pekee ndiye aliyefanya mbegu iote. Anayepanda mbegu ni sawa na yule anayemwagilia maji. Kila mmoja wao atapokea malipo yake kulingana na kazi yake. Sisi ni wafanyakazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu; ninyi ni jengo la Mungu.

10 Kwa neema niliyopewa na Mungu nilijenga msingi kama mjenzi hodari, na mtu mwingine ana jenga juu ya msingi huo. Lakini kila mmoja awe mwangalifu anavyojenga juu yake. 11 Kwa maana hakuna mtu anayeweza kuweka msingi mwingine isipokuwa ule uliokwisha jengwa, ambao ni Yesu Kristo. 12 Kama mtu ye yote atajenga juu ya msingi huu akitumia dhahabu, fedha, mawe ya tha mani, mbao, majani au nyasi, 13 kazi yake itaonekana; kwa kuwa ile siku itaidhihirisha kazi yake. Itadhihirishwa kwa moto, na moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu. 14 Kama alichojenga hakitaharibiwa kwa moto, atapokea tuzo. 15 Kama kazi ya mtu itateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini kama mtu aliyenusurika kwenye moto.

16 Je, hamjui kwamba ninyi ni Hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17 Kama mtu ye yote akiliharibu Hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa sababu Hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ni Hekalu hilo. 18 Mtu asijidanganye mwenyewe. Kama kuna mtu miongoni mwenu anadhani kuwa yeye ana hekima kwa kipimo cha nyakati hizi, basi afadhali awe mjinga ili apate kuwa na hekima ya kweli. 19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuuzi mbele za Mungu. Kama Maandiko yasemavyo, “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao.’ ’ 20 Na tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni bure.”

21 Kwa hiyo mtu asijivune kwa sababu ya watu. Kwa kuwa vitu vyote ni vyenu, 22 kama ni Paulo au Apolo au Petro au dunia au maisha au kifo, au wakati uliopo au wakati unaokuja, haya yote ni yenu; 23 na ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.

Walimu ni Watumishi tu wa Mungu

Ndugu zangu, nilipokuwa kwenu, sikuzungumza nanyi kama ninavyozungumza na watu wanaoongozwa na Roho. Nilizungumza nanyi kama watu wa kawaida wa duniani. Mlikuwa kama watoto katika Kristo. Mafundisho niliyowafundisha yalikuwa kama maziwa, siyo chakula kigumu. Nilifanya hivi kwa kuwa hamkuwa tayari kwa chakula kigumu. Na hata sasa hamjawa tayari. Bado hamwenendi katika Roho, mnaoneana wivu na mnabishana ninyi kwa ninyi kila wakati. Hii inaonesha kuwa bado mnazifuata tamaa zenu wenyewe. Mnaenenda kama watu wa kawaida wa ulimwengu huu. Mmoja wenu anasema, “Mimi ninamfuata Paulo,” na mwingine anasema, “Ninamfuata Apolo.” Mnaposema mambo kama haya, mnaenenda kama watu wa ulimwengu.

Je, Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Apolo na mimi si watumishi tu ambao Mungu alitutumia ili mmwamini Yesu Kristo. Kila mmoja wetu alifanya kazi aliyopewa na Bwana. Nilipanda mbegu na Apolo akamwagilia maji. Lakini Mungu ndiye aliyeiotesha na kuikuza. Hivyo aliyepanda na kuimwagilia si wa muhimu. Mungu ndiye wa muhimu, kwa sababu ndiye anayevifanya vitu viote vikue. Anayepanda na anayemwagilia maji wote wana nia moja. Na kila mmoja atalipwa kutokana na kazi yake yeye mwenyewe. Ninyi ni shamba la Mungu, ambamo tulifanya kazi pamoja kwa ajili yake.

Nanyi pia ni jengo la Mungu. 10 Nami kama mjenzi stadi nilijenga msingi wa nyumba hiyo kwa kutumia karama alizonipa Mungu. Wengine wanajenga pia katika msingi huo. Lakini kila mtu lazima awe mwangalifu kwa namna anavyojenga. 11 Yesu Kristo ndiye msingi uliokwishajengwa, na hakuna yeyote anayeweza kujenga msingi mwingine. 12 Watu wanaweza kujenga juu ya msingi huo kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, mbao, nyasi au majani. 13 Kila kazi atakayoifanya kila mtu itaonekana siku ya hukumu itakapofika, na itaonekana ilivyo mbaya au nzuri. Siku hiyo kila kazi ya mtu itajaribiwa kwa moto. 14 Mungu atampa thawabu mtu anayejenga juu ya msingi huu ikiwa kazi yake haitateketea kwa moto. 15 Lakini ikiwa itateketea atapata hasara. Lakini yeye mwenyewe ataokolewa, lakini itakuwa kama mtu anayeokolewa kutoka kwenye moto.

16 Hakika mnajua kuwa ninyi ni hekalu la Mungu na Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. 17 Ndiyo, ninyi nyote kwa pamoja ni Hekalu la Mungu. Na yeyote atakayeliharibu Hekalu la Mungu ataadhibiwa na Mungu, kwa sababu Hekalu la Mungu ni mali yake yeye mwenyewe.

18 Msijidanganye. Yeyote anayejiona kuwa ana hekima kwa viwango vya ulimwengu huu, basi na awe mpumbavu. Hiyo ndiyo njia pekee itakayomfanya kuwa na hekima. 19 Ninasema hivi kwa sababu hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu huwanasa katika mitego yao wenyewe wale wanaojidhania kuwa na hekima.”(A) 20 Pia Maandiko yanasema, “Bwana anajua mawazo ya wenye hekima. Anajua kuwa mawazo yao hayana maana.”(B) 21 Hivyo hakuna mtu yeyote duniani ambaye ninyi mnapaswa kujivunia. Kila kitu ni chenu: 22 Paulo, Apolo, Petro, ulimwengu, uzima, mauti, wakati uliopo na ujao, vyote hivi ni vyenu. 23 Ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.