Karama Za Roho Mtakatifu

12 Sasa kuhusu karama za Roho Mtakatifu ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu. Mnajua kwamba mlipokuwa hamumjui Mungu mlivutwa na kupotoshwa na sanamu bubu.

Kwa hiyo napenda mfahamu ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kukiri, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho Mtakatifu. Basi kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni mmoja. Pia kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni mmoja. Kisha kuna aina tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule anayeongoza kazi zote kwa kila mtu. Roho Mtakatifu hudhi hirishwa kwa kila mtu kwa faida ya wote.

Maana mtu mmoja hupewa neno la hekima na huyo Roho, na mwingine hupewa neno la ufahamu kutoka kwa Roho huyo huyo. Mtu mwingine hupewa imani na huyo Roho na mwingine karama za kuponya. 10 Huyo huyo Roho humpa mwingine uwezo wa kufanya miujiza, mwin gine unabii, mwingine uwezo wa kutofautisha kati ya roho mbalim bali, mwingine aina za lugha na mwingine uwezo wa kutafsiri lugha. 11 Lakini ni Roho huyo huyo mmoja anayefanya haya yote, naye hugawa karama kwa kila mtu, kama yeye mwenyewe apendavyo.

Mwili Mmoja, Viungo Vingi

12 Kama vile mwili ulivyo mmoja lakini una viungo vingi, na viungo vyote ingawa ni vingi vinafanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo na Kristo. 13 Kwa maana tumebatizwa na Roho mmoja katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wagiriki, kama ni watumwa au watu huru; nasi tumepewa tunywe, huyo Roho mmoja.

14 Mwili si kiungo kimoja, bali una viungo vingi. 15 Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si sehemu ya mwili.” Hiyo isingefanya huo mkono usiwe sehemu ya mwili. 16 Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si sehemu ya mwili.” Hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili. 17 Kama mwili mzima ungelikuwa jicho, ungelisikiaje? Au kama mwili wote ungelikuwa sikio, ungelinusa namna gani? 18 Lakini kama mwili ulivyo, Mungu alipanga viungo vyote katika mwili, kimoja kimoja, kama alivyopenda. 19 Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja mwili ungekuwa wapi? 20 Kama mwili ulivyo, kuna viungo vingi, lakini mwili ni mmoja.

21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sikuhitaji!” Na kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sikuhitaji!” 22 Kinyume chake, vile viungo vya mwili ambavyo vinaonekana kuwa dhaifu ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana. 23 Na vile viungo vya mwili ambavyo tunav iona havina heshima ndivyo tunavipa heshima ya pekee. Na vile viungo vya mwili ambavyo hatuwezi kuvionyesha, tunavitunza kwa adabu 24 ambayo vile viungo vyenye uzuri wa kuonekana havihi taji. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile visivyokuwa na heshima, 25 ili pasiwe na mga wanyiko katika mwili, bali viungo vyote visaidiane kwa usawa. 26 Kama kiungo kimoja cha mwili kikiteseka, viungo vyote vinateseka pamoja; kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote vinafurahi pamoja.

27 Basi ninyi ni mwili wa Kristo, na kila mmoja wenu ni kiungo cha huo mwili. 28 Na Mungu ameteua katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, kisha waponyaji, wasaidizi, watawala, wasemaji wa lugha mbalimbali. 29 Je, wote ni mitume? Au wote ni manabii? Wote ni walimu? Wote wanafanya miujiza? 30 Je, wote wana karama ya kuponya? Wote wanasema kwa lugha ngeni? Wote wanatafsiri lugha? 31 Basi takeni kwa moyo karama zilizo bora. Nami nitawaonyesha njia iliyo bora kupita zote.

Karama Kutoka kwa Roho Mtakatifu

12 Na sasa ninataka mwelewe kuhusu karama za Roho Mtakatifu. Mnayakumbuka maisha mliyoishi kabla hamjawa waamini. Mlipotoshwa na kuongozwa kuziabudu sanamu, ambazo hata kuzungumza haziwezi. Hivyo ninawaambia ya kwamba hakuna mtu anayezungumza kwa Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu alaaniwe.” Na hakuna anayeweza kusema “Yesu ni Bwana,” bila msaada wa Roho Mtakatifu.

Kuna karama mbalimbali za Roho, lakini zote zinatoka kwa Roho yule yule. Kuna namna mbalimbali za kutumika, lakini sote tunatumika kwa niaba ya Bwana yule yule. Na kuna namna ambazo Mungu hufanya kazi ndani yetu sote, lakini ni Mungu yule yule anayetenda kazi ndani yetu ili tutende kila kitu.

Kitu fulani kutoka kwa Roho kinaweza kuonekana ndani ya kila mtu. Roho humpa kila mtu hili ili awasaidie wengine. Roho humpa mtu fulani uwezo wa kuzungumza kwa hekima. Na Roho huyo huyo humpa mwingine uwezo wa kuzungumza kwa maarifa. Roho huyo huyo humpa mtu karama ya imani na humpa mwingine karama ya kuponya. 10 Roho humpa mtu nguvu ya kutenda miujiza, na humpa mwingine uwezo wa kutabiri, na mwingine uwezo wa kupambanua kujua kilichotoka kwa Roho na ambacho hakikutoka kwa Roho. Roho humpa mtu fulani uwezo wa kusema kwa lugha zingine tofauti, na humpa mwingine uwezo wa kufasiri lugha hizo. 11 Roho mmoja, Roho yule yule hufanya mambo yote haya. Roho ndiye huamua ampe nini kila mtu.

Mwili wa Kristo

12 Mtu ana mwili mmoja, lakini una viungo vingi. Kuna viungo vingi, lakini viungo vyote hivyo ni mwili mmoja. Kristo yuko vivyo hivyo pia. 13 Baadhi yetu ni Wayahudi na baadhi yetu si Wayahudi; baadhi yetu ni watumwa na baadhi yetu ni watu tulio huru. Lakini sisi sote tulibatizwa ili tuwe sehemu ya mwili mmoja kwa njia ya Roho mmoja. Nasi tulipewa[a] Roho mmoja.

14 Na mwili wa mtu una viungo zaidi ya kimoja. Una viungo vingi. 15 Mguu unaweza kusema, “Mimi si mkono, na hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kusema hivi hakutafanya mguu usiwe kiungo cha mwili. 16 Sikio linaweza kusema, “Mimi si jicho, hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kwa kusema hivi hakutafanya sikio lisiwe kiungo cha mwili. 17 Ikiwa mwili wote ungekuwa jicho, usingeweza kusikia. Ikiwa mwili wote ungekuwa sikio, usingeweza kunusa kitu chochote. 18-19 Ikiwa viungo vyote vya mwili vingekuwa kiungo kimoja, mwili usingekuwepo. Kama jinsi ilivyo, Mungu aliweka viungo katika mwili kama alivyotaka. Alikipa kila kiungo sehemu yake. 20 Hivyo kuna viungo vingi, lakini kuna mwili mmoja tu.

21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sikuhitaji!” Na kichwa hakiwezi kuuambia mguu, “sikuhitaji!” 22 Hapana, viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu zaidi, ndivyo vilivyo na umuhimu zaidi. 23 Na viungo ambavyo tunadhani kuwa vina umuhimu mdogo ndivyo tunavitunza kwa heshima kubwa. Na tunavitunza kwa kuvifunika kwa uangalifu maalum viungo vya mwili tusivyotaka kuvionesha. 24 Viungo vinavyopendeza zaidi visipofunikwa havihitaji matunzo haya maalum. Lakini Mungu aliuunganisha mwili pamoja na akavipa heshima zaidi viungo vilivyohitaji hadhi hiyo. 25 Mungu alifanya hivi ili mwili wetu usigawanyike. Mungu alitaka viungo vyote tofauti vitunzane kwa usawa. 26 Ikiwa kiungo kimoja cha mwili kinaugua, basi viungo vyote vinaugua pamoja nacho. Au ikiwa kiungo kimoja kinaheshimiwa, basi viungo vingine vyote vinashiriki heshima ya kiungo hicho.

27 Ninyi nyote kwa pamoja ni mwili wa Kristo. Kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo. 28 Na Mungu ameweka katika kanisa, kwanza, baadhi kuwa mitume, pili manabii, na tatu walimu. Kisha Mungu ametoa nafasi kwa wale wanaofanya miujiza, wenye karama ya uponyaji, wanaoweza kuwasaidia wengine, wanaoweza kuwaongoza wengine na wale wanaoweza kuzungumza kwa lugha zingine. 29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote hufanya miujiza? 30 Si wote wenye karama ya uponyaji. Si wote wanaozungumza kwa lugha zingine. Si wote wanaofasiri lugha. 31 Endeleeni kuwa na ari ya kuwa na karama za Roho mnazoona kuwa ni kuu zaidi. Lakini sasa ninataka kuwaonesha njia iliyo kuu zaidi.

Footnotes

  1. 12:13 tulipewa Au, “tulinyweshwa”.