Dhabihu Ya Kristo Ilikuwa Ya Mwisho

10 Basi kwa kuwa sheria ni kivuli tu cha mambo mema yajayo na wala si mambo yenyewe, haiwezi kamwe, kwa njia ya dhabihu zito lewazo mwaka hadi mwaka, kuwakamilisha wale wanaoabudu. Kama isingekuwa hivyo, dhabihu hizo zingekuwa hazitolewi tena. Maana hao waabuduo wasingalijiona tena kuwa wana hatia kwa ajili ya dhambi zao baada ya kutakaswa mara moja. Badala yake, dhabihu hizo zilikuwa ni ukumbusho wa dhambi mwaka hadi mwaka. Kwa maana damu ya mafahali na mbuzi, haiwezi kamwe kuondoa dhambi.

Kwa sababu hii, Yesu alipokuja duniani alisema: “Hukutaka dhabihu na sadaka bali umeniandalia mwili. Hukupendezwa na sadaka za kuteketezwa wala sadaka zitolewazo kwa ajili ya dhambi. Ndipo nikasema, ‘Nipo hapa, kama ilivyoandikwa katika gombo la sheria kunihusu; nimekuja kutimiza mapenzi yako wewe Mungu.’ ”

Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa wala sadaka zitolewazo kwa ajili ya dhambi hukutaka, wala huku pendezwa nazo,” ingawa hizi zilitolewa kwa mujibu wa sheria. Kisha akasema, “Niko hapa, nimekuja kutimiza mapenzi yako.” Anaweka kando ule utaratibu wa kwanza na kuanzisha utaratibu wa pili. 10 Na kwa mapenzi hayo, sisi tumetakaswa kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu, kwa wakati wote.

11 Kila kuhani husimama siku hadi siku akifanya huduma yake ya ibada na akitoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kuondoa dhambi. 12 Lakini Kristo alipokwisha kutoa dhabihu yake kwa ajili ya dhambi mara moja tu kwa wakati wote, aliketi upande wa kulia wa Mungu. 13 Tangu wakati huo anangoja mpaka Mungu atakapowafanya maadui zake kuwa kiti cha miguu yake. 14 Maana kwa dhabihu moja tu amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.

15 Roho Mtakatifu pia anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema: 16 “Hili ndilo agano nitakalofanya nao baada ya siku hizo, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao na kuziandika akilini mwao.” 17 Kisha anasema: “Dhambi zao na makosa yao sitayakumbuka tena kamwe.”

18 Basi, haya yakishasamehewa, hakuna tena dhabihu inayoto lewa kwa ajili ya dhambi.

Haja Ya Kuwa Imara

19 Kwa hiyo ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kuingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu, 20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake, 21 na kwa kuwa tunaye kuhani mkuu anayemiliki nyumba ya Mungu; 22 basi tumkaribie Mungu kwa moyo wa kweli na imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya na miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23 Tushikilie kwa makini tumaini tunalokiri kwa maana yeye ali yeahidi ni mwaminifu. 24 Na tujishughulishe kutafuta jinsi ya kuhimizana katika kuonyeshana upendo na kutenda mema. 25 Tusiache kukutana pamoja, kama wengine wanavyofanya, bali tutiane moyo, hasa zaidi tunapoona siku ile ikikaribia.

Hatari Ya Kukufuru

26 Kama tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kupokea na kufahamu ile kweli, hakuna tena dhabihu iliyobaki inayoweza kutolewa kwa ajili ya dhambi. 27 Kinachobakia ni kungojea kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza maadui zake. 28 Mtu aliyevunja sheria ya Mose aliuawa pasipo huruma kwa usha hidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani zaidi anastahili kupewa mtu ambaye anamdharau na kum kataa Mwana wa Mungu, na ambaye anaona kuwa damu ya agano iliyom takasa si kitu, na ambaye amemtukana Roho wa neema? 30 Kwa maana tunamjua yeye aliyesema, “Kulipiza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipiza.” Pia alisema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha.

32 Kumbuka siku zile za mwanzo baada ya kupokea mwanga, jinsi mlivyovumilia mapambano makali na mateso. 33 Wakati mwin gine mlitukanwa na kuteswa hadharani; wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa hivyo. 34 Mliwaonea huruma waliokuwa kifungoni, na mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu kwa maana mlifahamu kwamba mlikuwa na mali bora zaidi inay odumu.

35 Kwa hiyo msitupe tumaini lenu, ambalo litapewa tuzo kubwa. 36 Mnahitaji kuvumilia ili mkisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi. 37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo tu yeye anayekuja atakuja , wala hatakawia; 38 lakini mtu wangu mwenye haki ataishi kwa imani, na akirudi nyuma sitapendezwa naye.”

39 Lakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaorudi nyuma wakaangamizwa, bali sisi ni miongoni mwa wanaoamini wakaokolewa.