Watoto Wa Mungu Wanavyopaswa Kuishi

Tazameni jinsi Baba alivyotupenda mno, hata tukaitwa watoto wa Mungu! Na hivyo ndivyo tulivyo. Watu wa ulimwengu hawatutambui kwa sababu hawakumjua Mungu. Wapendwa, sisi sasa tu wana wa Mungu. Tutakavyokuwa baadaye haijulikani bado, lakini tunajua kwamba Kristo atakapotokea, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.

Kujitakasa Na Kuacha Dhambi

Na kila mtu mwenye tumaini hili hujitakasa, kama yeye mwe nyewe alivyo mtakatifu.

Kila atendaye dhambi ana hatia ya kuvunja sheria; maana dhambi ni uvunjaji sheria. Mnajua kwamba Kristo alikuja kuondoa dhambi naye hana dhambi yo yote. Hakuna mtu anayedumu ndani ya Kristo ambaye anatenda dhambi; na mtu ye yote anayetenda dhambi, huyo hajapata kumwona Kristo wala kumjua.

Watoto wadogo, mtu asije akawadanganya. Kila atendaye haki ni mwenye haki, kama Kristo alivyo wa haki. Kila atendaye dhambi ni wa shetani; kwa maana shetani ametenda dhambi tangu mwanzo. Mwana wa Mungu alikuja ili aziangamize kazi za shetani.

Mtu aliyezaliwa na Mungu haendelei na tabia ya kutenda dhambi, kwa maana ana asili ya Mungu; hawezi kuendelea kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu.

Kutenda Haki Na Kupendana

10 Na hivi ndivyo tunavyoweza kutambua wazi kati ya walio watoto wa Mungu na walio watoto wa shetani. Mtu ye yote asiyet enda lililo haki si wa Mungu; wala asiyempenda ndugu yake si wa Mungu. 11 Na ujumbe mliosikia tangu mwanzo ndio huu: kwamba tupen dane. 12 Msiwe kama Kaini ambaye alikuwa wa yule mwovu akamwua ndugu yake. Na kwa nini alimwua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu lakini matendo ya nduguye yalikuwa ya haki.

13 Ndugu zangu, msishangae watu wa ulimwengu wakiwachukia. 14 Tunajua hakika kwamba tumevuka kutoka kwenye kifo na kuingia kwenye uzima kwa maana tunawapenda ndugu zetu. Asiye na upendo anaishi katika kifo. 15 Kila anayemchukia ndugu yake ni mwuaji, na kama mjuavyo, hakuna mwuaji ambaye ana uzima wa milele ndani yake.

16 Na tumeujua upendo kwa sababu Kristo alitoa maisha yake kwa ajili yetu. Na sisi tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu. 17 Lakini ikiwa mtu ana mali za hapa duniani na akamwona ndugu yake ana shida lakini akawa na moyo mgumu wala asimhurumie, mtu kama huyo anawezaje kusema anao upendo wa Mungu? 18 Wanangu, upendo wetu usiwe wa maneno matupu, bali upendo wetu udhihirishwe kwa vitendo na kweli.

19 Hivi ndivyo tutakavyoweza kuwa na hakika kwamba sisi ni wa kweli na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu 20 hata kama dhamiri zetu zitatuhukumu; kwa maana tunajua kwamba Mungu ni mkuu kuliko dhamiri zetu, naye anajua kila kitu. 21 Wapendwa, ikiwa dhamiri zetu hazituhukumu, tuna ujasiri mbele za Mungu; 22 nasi tunapokea kutoka kwake lo lote tuombalo kwa kuwa tunatii amri zake na kufanya yampendezayo. 23 Na amri yake ndio hii: tuliamini jina la Mwanae Yesu Kristo na kupendana, kama alivyotu agiza. 24 Wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Na hivi ndivyo tunavyojua kwamba anaishi ndani yetu: tunajua kwa njia ya yule Roho aliyetupatia.