23 Paulo akawakazia macho wajumbe wa baraza, akasema, “Ndugu zangu, mimi nimeishi nikiwa na dhamiri safi kabisa siku zote mbele za Mungu, mpaka leo.” Kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi mdomoni. Ndipo Paulo akasema, “Mungu atakupiga, wewe ukuta uliopakwa chokaa! Unawe zaje kusikiliza kesi hii kwa mujibu wa sheria, na hapo hapo, kinyume cha sheria, unaamuru nipigwe?” Wale watu waliokuwa wamesimama karibu wakamwambia Paulo, “Mbona unamtukana kuhani mkuu wa Mungu?” Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye ni kuhani mkuu. Kwa maana Maandiko yanasema, ‘Usimseme vibaya kiongozi wa watu wako.’ ” Paulo alipotambua ya kuwa baadhi ya wajumbe wa baraza walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo alisema nao kwa sauti kubwa, “Ndugu zangu! Mimi ni Mfarisayo, mtoto wa Mafarisayo; na hapa nimeshitakiwa kuhusu tumaini juu ya ufufuo wa wafu.” Aliposema haya, Mafarisayo na Masadukayo wakafarakana na baraza zima likagawanyika. Kwa maana Masadukayo wanaamini kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho; lakini Mafarisayo wanaamini haya yote. Kelele zikazidi sana; na baadhi ya waandishi wa sheria wa upande wa Mafarisayo, wakasimama wakiwapinga wengine wakasema, “Hatuoni kosa lo lote alilofanya mtu huyu! Huenda ikawa malaika au roho amezungumza naye kweli!” 10 Mabishano yalipozidi kuwa makali, yule jemadari aliogopa kuwa wangeweza kumrarua Paulo vipande vipande. Kwa hiyo akaamuru askari wakamtoe Paulo alipokuwa, arudishwe kwenye ngome ya jeshi. 11 Usiku uliofuata, Bwana akamtokea Paulo akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, itakubidi unishuhudie na huko Rumi pia.”

Njama Za Wayahudi Kumwua Paulo

12 Kulipopambazuka Wayahudi wakala njama ya kumwua Paulo. Wakaweka nadhiri kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo. 13 Waliofanya mpango huu walikuwa zaidi ya watu arobaini. 14 Wakaenda kwa kuhani mkuu na wazee wakasema, “Tumeweka nad hiri ya pamoja kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tumwue Paulo. 15 Kwa hiyo ninyi pamoja na baraza, pelekeni ombi kwa jemadari ili Paulo aletwe barazani, mtoe udhuru kwamba mnataka kuchunguza kesi yake kwa usahihi zaidi. Sisi tutakuwa tayari kumwua hata kabla hajakaribia kufika hapa.” 16 Basi kumbe binamu yake Paulo alisikia kuhusu mpango huu. Akaenda katika ngome ya jeshi akamweleza Paulo mambo haya. 17 Paulo akamwita mmoja wa wale maaskari akamwambia, “Mchukue kijana huyu kwa jemadari, ana neno la kumwambia.” 18 Yule askari akamchukua yule kijana mpaka kwa jemadari akamwambia, “Yule mfungwa Paulo aliniita akaniambia nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukuambia.” 19 Yule jemadari akamchukua yule kijana kando akamwuliza, “Unataka kuniambia nini?” 20 Naye akasema, “Wayahudi wameku baliana wakuombe kesho umpeleke Paulo kwenye Baraza lao kwa kisingizio kwamba wanataka kuchunguza kesi yake kwa uangalifu zaidi. 21 Lakini usikubali ombi lao kwa maana zaidi ya watu aro baini wamekula njama kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wamwue Paulo nao wamejiweka tayari kumvizia ukishakubali ombi lao.” 22 Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende, akamwonya akisema, “Usimwambie mtu ye yote kwamba umenieleza habari hizi.”

Paulo Apelekwa Kaisaria Kwa Gavana Feliksi

23 Yule jemadari akawaita maaskari wawili akawaambia, “Tay arisheni askari mia mbili watakaokwenda Kaisaria pamoja na askari wa farasi sabini, na askari wa mikuki mia mbili; nanyi muwe tay ari kuondoka leo saa tatu za usiku. 24 Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mumpeleke salama mpaka kwa gavana Feliksi.” 25 Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo: 26 “Mimi Klaudio Lisia, nakuandikia wewe gavana mtukufu Feliksi. Salamu. 27 Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakawa kar ibu kumwua, ndipo mimi nilipofika na askari wangu nikamwokoa kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raia wa Kirumi. 28 Nami nikampeleka mbele ya baraza lao ili nipate kujua kosa alilofanya. 29 Ndipo nikagundua ya kuwa alikuwa anashtakiwa kuhusu sheria yao, lakini hakuwa na kosa la kustahili kifo au kifungo. 30 Lakini nilipata habari kwamba kuna mpango wa kumwua nikaamua nimpeleke kwako mara moja, nikawaamuru washitaki wake walete mashtaka yao kwako.” 31 Basi wale askari wakamchukua Paulo usiku wakampeleka mpaka Antipatri kama walivyoamriwa. 32 Kesho yake wakarudi kituoni wakawaacha wale askari wa mikuki waendelee na safari pamoja na Paulo. 33 Walipofika Kaisaria walimpa Liwali ile barua na pia wakamkabidhi Paulo kwake. 34 Alipokwisha soma ile barua, alimwuliza Paulo ametoka jimbo gani. Alipofahamishwa kuwa anatoka Kilikia 35 alisema, “Nitasikiliza kesi yako mara tu washtaki wako watakapofika.” Akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi katika ikulu ya Herode.