Mpendwa Teofilo, Katika Kitabu changu cha kwanza nilikuan dikia kuhusu mambo yote aliyotenda Yesu, hadi wakati alipopaa mbinguni. Kabla hajachukuliwa juu, aliwapa mitume wake maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Alijionyesha kwao akiwa hai muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake. Akawahakikishia kwa njia nyingi ya kuwa ni yeye na akaongea nao kuhusu Ufalme wa Mungu.

Wakati mmoja alipokuwa nao, aliwapa amri hii, “Msiondoke Yerusalemu, mpaka mtakapopokea ahadi aliyotoa Baba, ambayo mmeni sikia nikiizungumzia. Kwa maana Yohana aliwabatiza kwa maji lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

Yesu Apaa Mbinguni

Mitume walipokutana na Yesu walimwuliza, “Bwana, wakati huu ndipo utawarudishia Waisraeli ufalme ?”

Yesu akawaambia, “Si juu yenu kufahamu wakati na majira ambayo yamewekwa na Baba kwa mamlaka yake. Lakini mtapokea nguvu akishawajilia Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu na Yudea yote na Samaria, hadi mwisho wa dunia.”

Baada ya kusema haya, wakiwa wanatazama, alichukuliwa juu, na wingu likamficha wasimwone tena. 10 Walikuwa bado wakikaza macho yao mawinguni alipokuwa akienda, ndipo ghafla, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe walisimama karibu nao, 11 wakasema, “Ninyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama hapa mkitazama mbin guni? Yesu huyu huyu aliyechukuliwa mbinguni atarudi tena kama mlivyomwona akienda mbinguni.”

12 Ndipo mitume waliporudi Yerusalemu kutoka mlima wa Mizeituni ulioko umbali wa kama kilometa moja kutoka mjini. 13 Walipoingia mjini Yerusalemu walikwenda katika chumba cha ghorofani walipokuwa wakiishi: Petro, Yohana, Yakobo na Andrea, Filipo, Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo na Simoni aliyeitwa Mzalendo, na Yuda mwana wa Yakobo.

14 Hawa wote waliamua kwa kauli moja kutumia muda wao wote kusali, wakiwa pamoja na wale akina mama, Mariamu mama yake Yesu pamoja na ndugu zake.

15 Ilikuwa ni katika siku hizo ambapo Petro alisimama kati ya waamini wote, watu wapatao mia moja na ishirini, 16 akasema, “Ndugu zangu, ilibidi Maandiko ambayo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu, yatimie. 17 Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.” 18 Yuda alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na uovu wake na akiwa huko shambani alianguka kifudifudi akapasuka na matumbo yote yakatoka nje. 19 Kila mkazi wa Yerusalemu alisikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani ‘shamba la Damu.’ 20 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Zab uri, ‘Mahali pake pasiwe na kitu wala asiwepo mtu atakayekaa hapo,’ na, ‘Nafasi yake ichukuliwe na mwingine.”’

Mathiya Achaguliwa

21 “Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine kati ya wale ambao wamekuwa pamoja nasi 22 tangu wakati Yesu alipobatizwa na Yohana mpaka siku aliyochukuliwa mbinguni. Mmoja wao inabidi aun gane nasi kama shahidi wa ufufuo wa Yesu.”

23 Wakapendekeza majina ya watu wawili. Yusufu, aitwaye Barsaba, pia alijulikana kama Yusto, na Mathiya. 24 Wakaomba, “Bwana ujuaye mioyo ya watu wote, tunakuomba utuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25 achukue nafasi ya huduma na utume ambayo Yuda aliiacha akaenda panapomstahili.”

26 Kisha wakapiga kura na Mathiya akachaguliwa. Basi akain gizwa katika kundi la wale mitume kumi na mmoja.